Na Hassan Abbas, Addis Ababa
MAANDALIZI ya Mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) zinazoshiriki katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) yameanza jijini hapa ambapo nchi za Tanzania na Zambia zinatarajiwa kuwasilisha Ripoti zao za Hali ya Utawala Bora ili zijadiliwe.
Mpango wa APRM uliasisiwa miaka 10 iliyopita na Wakuu wa Nchi za Afrika kwa lengo la kuanzisha taasisi itakayokuwa na majukumu ya kufanya tathmini za mara kwa mara za hali ya utawala bora miongoni mwa nchi wanachama ili kuwashirikisha wananchi wao katika kujikosoa na kujisahihisha.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Makao Makuu ya APRM, mikutano hiyo ya APRM ambayo kwa kawaida hufanyika sanjari na Mikutano ya AU, unaanza mjini hapa leo Jumatano Januari 23, 2013 kwa mkutano wa 59 wa Jopo la Watu Mashuhuri linalosimamia mchakato wa APRM kukutana.
Mkutano huo utafuatiwa na mkutano wa wabia wanaoshirikiana na mchakato wa APRM na Ijumaa, kitafanyika kikao cha maandalizi kabla ya Jumamosi kufanyika Mkutano wa Wakuu wa Nchi.
Taarifa iliyotolewa hivi karibu na APRM Makao Makuu, ilithibitisha kuwa Ripoti ya tathmini ya Tanzania iliyosheheni maoni ya wadau wa utawala bora Tanzania na majibu ya Serikali itawasilishwa katika kikao hicho.
“Ripoti ya Hali ya Utawala Bora ya Tanzania baada ya kukamilishwa inatarajiwa kujadiliwa mbele ya kikao cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika wanachama wa APRM kitakachofanyika Januari 26, 2013,” ilisema taarifa hiyo ya APRM makao makuu.
Akizungumza na watendaji wa APRM Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo, Rais Jakaya Kikwete alikaririwa jijini Dar es Salaam wiki iliyopita akisisitiza kuwa Serikali yake inaamini kuwa mchakato wa APRM hapa nchini ulifanyika kwa uwazi na kwamba yuko tayari kwenda kufanyiwa tathmini na wakuu wenzake wan chi za AU.