MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) inayoshirikisha timu 27 inaanza kutimua vumbi kesho (Mei 10 mwaka huu) katika vituo vitatu vya Morogoro, Mbeya na Shinyanga kwa mechi mbili kila siku. Kundi A ambalo mechi zake zinachezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, African Sports ya Tanga itacheza na Kiluvya United FC ya Pwani saa 8 mchana wakati saa 10 jioni ni Mji Mkuu FC (CDA) ya Dodoma dhidi ya Pachoto Shooting Stars ya Mtwara.
Jumapili (Mei 11 mwaka huu) katika kundi hilo kutakuwa na mechi kati ya Bulyanhulu FC (Shinyanga) na Kariakoo SC (Lindi) itakayoanza saa 8 mchana wakati saa 10 jioni ni Navy FC (Dar es Salaam) na Abajalo FC pia ya Dar es Salaam. Kundi B katika Uwanja wa CCM Vwawa uliopo Mbozi jijini Mbeya litaanza ligi kwa mechi kati ya Ujenzi (Rukwa) na Volcano FC (Morogoro) saa 8 mchana wakati saa 10 jioni ni AFC ya Arusha na Panone FC ya Kilimanjaro.
Mei 11 mwaka huu saa 8 mchana ni Mpanda United ya Katavi na Magereza ya Iringa wakati Tanzanite (Manyara) na Njombe Mji (Njombe) zenyewe zitaumana kuanzia saa 10 jioni. Simiyu United ya Simiyu na Mvuvumwa FC (Kigoma) ndizo zitakazoanza kucheza saa 8 mchana katika kundi C linalotumia Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Saa 10 jioni ni mechi kati ya Wenda FC ya Mbeya na mabingwa wa Mkoa wa Kagera, Eleven Stars FC.
Jumapili (Mei 11 mwaka huu), mechi za kundi hilo zitakuwa Singida United (Singida) na Mbao FC ya Mwanza kuanzia saa 8 mchana wakati jioni ni pambano kati ya mabingwa wa Mkoa wa Mara, JKT Rwamkoma FC na Geita Veterans FC ya Geita. Ligi hiyo itamalizika Juni 2 mwaka huu ambapo timu itakayoongoza kila kundi itapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2014/2015.
MAKOCHA NGORONGORO HEROES, EAGLES KUTETA
Makocha wa timu za Tanzania (Ngorongoro Heroes), John Simkoko na Nigeria (Flying Eagles), Manu Garba wanakutana na waandishi wa habari kuzungumzia mikakati yao kwa ajili ya mechi ya Jumapili. Mkutano huo utafanyika kesho (Mei 10 mwaka huu) kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuanzia saa 5 kamili asubuhi.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 itafanyika Jumapili (Mei 11 mwaka huu) saa 10 kamili jioni katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Fainali hizo za 19 za Afrika zitafanyika mwakani nchini Senegal zikishirikisha timu saba zitakazofuzu kwenye mechi za mchujo, na Senegal wanaoingia moja kwa moja kutokana na kuwa wenyeji.
Wakati Ngorongoro Heroes leo (Mei 9 mwaka huu) saa 10 jioni itafanya mazoezi yake Uwanja wa Azam uliopo Chamazi, Flying Eagles yenyewe muda huo huo itafanya mazoezi Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 2,000 kwa sehemu zote wakati upande wa VIP itakuwa sh. 5,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mechi katika magari maalumu.