Michuano ya kuwania Kombe la Kagame iliyofanyika nchini kuanzia Juni 25 hadi
Julai 10 mwaka huu imekwenda vizuri huku timu za Tanzania, Yanga na Simba
zikifanya vizuri kwa kufika hatua ya fainali. TFF tunazipongeza timu hizo kwa
uwakilishi mzuri ziliotupa, hasa Yanga kwa kuibuka mabingwa.
Shukrani za pekee tunatoa kwa mashabiki waliojitokeza kushuhudia mechi za
michuano hiyo zilizofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Uwanja wa
Jamhuri mjini Morogoro. Mahudhurio ya washabiki katika mechi zote yaliingiza
jumla ya sh. bilioni 1.073. Fedha hizo zimetuwezesha kulipia gharama zote za
mashindano.
Pia tunatoa shukrani kwa wadau wengine waliowezesha mashindano hayo kufanikiwa
wakiwemo wadhamini, hoteli, kampuni za usafiri, ulinzi, Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, waandishi wa habari Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) na klabu ya TCC Chang’ombe kwa kutoa viwanja vya mazoezi na Serikali kwa
kutoa Uwanja wa Taifa.
Hoteli hizo ni Safina, Landmark, Lunch Time, Marriot, Paradise City, Valentino,
Spice Inn, Blue Pearl, Akubu na Jangwani Plaza za Dar es Salaam. Oasis, Top Life
na Kingston za Morogoro.,
Licha ya mafanikio hayo, tunawaomba radhi mashabiki kutokana na kukatika umeme
kwenye Uwanja wa Taifa baada ya mechi ya fainali kati ya Yanga na Simba. Tukio
hilo lilitokea wakati wa kukabidhi zawadi kwa timu mbalimbali zilizofanya vizuri
katika mashindano hayo.
USAJILI WA WACHEZAJI
Kipindi cha uhamisho wa wachezaji kwa msimu wa mwaka 2011/2012 kinamalizika
Julai 15 mwaka huu wakati mwisho wa usajili ni Julai 20 mwaka huu.
Kwa upande wa klabu za Ligi Kuu, usajili wao unaanzia kwa timu za pili (U20),
hivyo kwanza zinatakiwa kukabidhi usajili wa timu hizo na baadaye za timu zao za
kwanza (senior). Klabu zote za Ligi Kuu tayari zina passwords zao kwa ajili ya
kufanya usajili wa wachezaji wa kigeni.
Dirisha dogo la usajili litafunguliwa tena Novemba 1 hadi 30 mwaka huu.
Tunazikumbusha timu zote za Ligi Kuu kuwasilisha majina ya viwanja ambavyo
zitatumia kwa ajili ya ligi hiyo ambayo itaanza Agosti 20 mwaka huu.
Klabu ambazo zimewasilisha maombi ya viwanja ambavyo zitatumia ni Mtibwa Sugar
(Manungu), Azam (Chamazi), Ruvu Shooting Stars (Mlandizi), Coastal Union
(Mkwakwani), Toto Africans (CCM Kirumba), Oljoro JKT (Kumbukumbu ya Sheikh Amri
Abeid Kaluta), Polisi Tanzania (Jamhuri, Dodoma) na Kagera Sugar (Kaitaba).
Klabu ambazo bado hazijawasilisha viwanja vyao ni Yanga, Simba, Moro United,
Villa Squad, JKT Ruvu na African Lyon. Timu hizo zinatakiwa kutuma majina ya
viwanja vyao haraka, kwani kabla ya kuruhusiwa kutumika ni lazima vithibitishwe
na Kurugenzi ya Ufundi ya TFF.
U23 v SHELISHELI
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 23, Jamhuri
Kihwelo ametangaza orodha ya wachezaji 21 kwa ajili ya mechi za kirafiki dhidi
ya timu ya taifa ya Shelisheli.
Mechi hizo mbili zitachezwa Julai 27 na 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu
ya Sheikh Amri Abeid Kaluta jijini Arusha.
Wachezaji hao ni Juma Abdul (Mtibwa Sugar), Himid Mao (Azam), Babu Ally
(Morani), Shabani Kado (Yanga), Salum Abubakar (Azam), Godfrey Wambura (Simba),
Jabir Aziz (Azam), Seif Juma (Ilala), Khamis Mcha (Azam), Shomari Kapombe
(Simba), Jackson Wandwi (Azam).
Wengine ni Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Thomas Ulimwengu (Humbarg SV, Ujerumani),
Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Mohamed Soud (Toto Africans), Jamal Mnyate (Azam),
Awadh Juma (Moro United), Salum Kanoni (Simba), Salum Telela (Yanga), Samuel
Ngasa (African Lyon) na George Mtemahanji (Modeva FC, Italia).