Na Anna Nkinda – Maelezo
WADAU wa michezo, wapenzi wa amani, afya na maendeleo ya vijana nchini wameshauriwa kuwekeza zaidi katika michezo kwani inamuepusha mtoto na vishawishi vingi vya afya ya uzazi.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Daud Nasib wakati akiishukuru Kampuni ya Montage Tanzania kwa kutoa vifaa vya michezo kwa ajili ya shule ya Sekondari ya wasichana ya WAMA- Nakayama iliyopo Rufiji mkoani Pwani.
Nasibu alisema kama wadau hao watahitaji kupata msaada wa kuzitambua shule zenye mahitajia maalum kama ya WAMA – Nakayama watawasaidia kuzitambua shule hizo.
Alisema mchango huo ni mzuri kwani unahamasisha umuhimu wa michezo shuleni kwa kuwa michezo ni muhimu kwa afya ya akili na humuwezesha kijana kukua vizuri na kwa usalama pale atakapokuwa mwanamichezo kutamsaidia kujiepusha na mambo mengi yanayoweza kumletea tabu katika maisha yake.
Akiongea mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo vya michezo Teddy Mapunda ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo alisema wametekeleza yale ambayo waliyaahidi walipotembelea shule hiyo wakati wa sherehe za sikukuu ya Eid Mubarak alisikia watoto wanapenda kushiriki katika michezo lakini kulikuwa na upungufu wa vifaa vya michezo na kuamua kuwasaidia vifaa hivyo.
Teddy aliwaomba wanafunzi hao kutumia vipindi vya michezo kucheza kwa bidii kwani michezo ni ajira, uhai na inaongeza akili shuleni pia inaleta amani na kujenga urafiki na ushirikiano.
Kwa upande wake Mwalimu wa michezo wa shule hiyo Mbwana R. Mbwana alishukuru kwa jezi na mipira waliyopewa kwa nia ya kuendeleza michezo shuleni hapo kwani itawasaidia kushiriki michezo mbalimbali katika ngazi ya shule na UMISETA. wanakabiliwa na ukosefu wa vuafaa vya michezo shuleni hapo.
Mwalimu Mbwana alisema mwaka juzi katika mashindano ya UMISETA walipeleka wanafunzi saba katika ngazi ya mkoa huko kibaha na mwaka jana walipeleka wawili ila kupatikana kwa vifaa hivyo anaamini miaka ijayo watapeleka wanafunzi wengi zaidi na kufanya vizuri zaidi.
Kampuni ya Montage Tanzania imetoa msaada wa mipira ya kuchezea mpira wa miguu mitano na pete minne, jezi za mpira wa pete 18 na mpira wa miguu 26 na jezi za mlinda mlango wa mpira wa miguu mbili.