*Ngoma Africa Band wawakivutio kwa waheshimiwa
DESEMBA 9 na 10, 2011 Watanzania waishio Ujerumani na nchi jirani wakishirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Ujerumani, walijikuta wakilitingisha Jiji la Berlin katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Taarifa zinasema sherehe hizo zilizoongozwa na Balozi, Ngemela na maofisa wengine wa ubalozi akiwemo, Ali Siwa zilianzia katika Ukumbi wa Martim, na kuhudhuriwa na mkusanyiko wa mabalozi wa nchi mbalimbali, viongozi wa ngazi za juu wa Serikali ya Ujerumani, Watanzania, wawakilishi wa mashirika NGO’s, na marafiki wahisani wa Tanzania.
Waalikwa hao walisherehekea na kuipongeza Tanzania kwa kufikia miaka 50 ya Uhuru kwa amani, huku zikimiminika salaam za pongezi kwa hatua hiyo na hasa kwa kitendo cha kudumisha amani barani Afrika, ambayo wananchi wake wanaishi kwa amani na upendo.
Ngoma Africa Band aka ‘FFU’ chini ya uongozi wa Ras Makunja alimaarufu Kamanda wa FFU, iliporomosha muziki na kufanikiwa kuwachanganya wanadiplomasia na wadau waliyoshiriki katika hafla, hasa kwa kutumia vibao vyao vipya vilivyotungwa mahususi kwa ‘Shangwe za miaka 50 ya Uhuru.
Pia sherehe hizo ziliambata na ufunguzi wa Chama cha Watanzania Ujerumani (UTU) ambacho kilifunguliwa rasmi Desemba 10, 2011 na Balozi Ngemera ambaye ni mwanzilishi wa umoja huo ambao ndio mwavuli wa Watanzania wote waishio Ujerumani. Umoja huo pia umesajaliwa na Serikali ya Ujerumani kama NGO’s chini ya Mwenyekitiki wake, Mfundo P. Mfundo.