Ndugu wanamabadiliko,
Mimi nakubaliana na wale wanaosema Dk. Nchimbi alialikwa jangwani. Nimelazimika kuingilia kati na kutoa ushahidi wa kiapo kwa vile naona kama vile ukweli hausemwi. Maoni yangu ni kwamba watu wakubali ukweli hata kama unauma na ukweli wenyewe unapatikana kutokana na ushaidi wa mazingira (circumstantial evidence):
KIAPO CHENYEWE;
MIMI Nyaronyo Mwita Kicheere, mtu mzima, mpagani na mkazi wa Tungi, Kigamboni, Dar es Salaam, Tanganyika territory (pamoja na sehemu za Ziwa Nyasa), NAAPA kwa mizimu ya Nyamongo na KUTAMKA yafuatayo:
1. KWAMBA mimi Nyaronyo Mwita Kicheere, nilikuwepo, nilishiriki na nilichunguza kwa makini nyendo za watu fulani fulani kwenye maandamano ya wanahabari yaliyofanyika jumanne wiki hii kwa hiyo nafahamu ukweli wa haya ninayoyaeleza hapa chini.
2. KWAMBA baada ya kuandamana kutoka ofisi za Channel Ten hadi viwanja vya jangwani hatukukuta maandalizi yoyote ya maana pale viwanjani jangwani kwa maana kwamba hakukuwepo jukwaa wala vipaza sauti.
3. KWAMBA muda mfupi tu baada ya kuwasili zilisikika sauti na minong’ono ya chinichini hasa ya akina mama wakipinga ujio wa dakitari wetu mtukuka nchimbi na kwamba kwa sababu ya ufupi wake nchimbi hakuwa ameonekana kwa wengi wala kufahamika kuwa alikuwapo.
4. KWAMBA mimi binafasi nilichukua jukumu la kuwahoji wale wanahabari wa kike, kama huyo nchimbi wanayemlalamikia ni nani, na yuko wapi, na kaja kufanya nini pale jangwani kama yeye si mwanahabari.
5. KWAMBA wanahabari wale wa kike walinielekeza mimi pamoja na wenzangu tuliokuwapo jirani nao mtu waliyedai ni dakitari mtukuka nchimbi na wakadai kuwa mtu yule hakuwa na lolote la kuuambia ummati ule wa wanahabari kwa sababu wauaji ni serikali na Nchimbi ni sehemu ya serikali.
6. KWAMBA mimi pamoja na wenzangu tuliokuwa tumesimama jirani na wanahabari wale wa kike tulisaidia kusema na kupaza sauti kuwa nchimbi hahitajika kwenye mkutano ambao serikali ilikuwa inalaaniwa kwa vitendo vya watendaji wake na hasa polisi ambao wanapaswa kulinda amani, mali na uhai wa raia lakini wao wanashiriki kuua!
7. KWAMBA Nchimbi kwa kujiamini kabisa alitukonyeza kuashiria kufahamiana sana na sisi na kwamba yeye ni mwenzetu. zipo ishara, vitendo na mwonekano (body language) vinavyoashiria kuwa mhusika ni mwenyeji tena alwatan na hivyo hababaiki wala kuterereka na yanayotokea mfano ukonyezaji.
8. KWAMBA kitendo cha kutukonyeza badala ya kuondoka viwanjani jangwani kilituudhi wandishi na hasa wanahabari wa kike ambao waliongeza sauti zao kumkana nchimbi na kumtaka aondoke jangwani ili kuwaacha wanahabari waomboleze peke yao kifo cha mwenzao.
9. KWAMBA pamoja na kelele za “Nchimbi ondoka kuongezeka”, Msemaji wa Jukwaa la Wahariri (Charles Misango) alipopanda kwenye rundo la udongo lililogeuzwa jukwaa kutokana na kutokuwepo maandalizi ya maana naye nchimbi alimfuata jirani na kupanda jukwaa lile la rundo la udongo kama mtu aliye tayari kutoa hotuba.
10. KWAMBA hapo ndipo uzalendo ulipowashinda wandishi na kilichofuata ni biashara inayofahamika kwetu wote wanahabari, mashushushu (ambao siku ile hawakuwa wanahesabika pale jangwani kwa wingi wao), mapolisi na wananchi kwa ujumla.
11. KWAMBA baada ya sakata lile la kumwondoa Nchimbi mkutanoni na akaondoka kwa aibu zote zinazoweza kuelezeka, wandishi wa ITV walimfuata pembeni na kumhoji na baadaye siku hiyo kumwonyesha na kumtangaza nchimbi eti wakitaka kujua sababu za yeye kuvamia maandamano ya wanahabari.
12. KWAMBA kwa uelewa wa mtu wa kawaida, ITV wanashukiwa kuhusika na kumwalika nchimbi jangwani. Kwa nini wamfuate mtu kumhoji baada ya kumtimua? Unamtimua wa nini kama unamhoji na kumtangaza si bora ungemwacha basi akahutubia wandishi halafu mkapata habari ya kuonyesha na kutangaza kama lengo na nia yenu ITV ilikuwa habari za nchimbi na siyo maombolezo ya Mwangosi? Kitendo hiki hakivumiliki na kilitudhalilisha sana wanahabari. Mnamfukuzaje mtu halafu mnamkimbilia kumlamba miguu?
13. KWAMBA ninakumbuka kuwa hii si mara ya kwanza ITV kufanya jambo la kinafiki na la hovyo kama hili. huko nyuma, wandishi waliwahi kukubaliana kutomquote wala kumwandika Waziri Mkuchika hata angefanya nini duniani hapa. lakini siku mkuchika alipokuwa anahutubia jambo fulani na akatamka mema kadhaa kumhusu mwenyekiti wa IPP R.A.Mengi maamuzi ya wanahabari yalitupiliwa mbali na mkuchika akatangazwa na kuonyeshwa kwenye runinga za ITV na IPP akimsifia bwana mkubwa bila kujali mgomo uliokuwepo!
14. KWAMBA pamoja na ITV mtu mwingine ninayemtuhumu na kumshutumu kwa kumwalika nchimbi ni katibu wa Jukwaa la Wahariri Bw. Nevil Meena. huyu bwana alitoa hotuba nzuri sana lakini akamalizia hotuba yake na maneno mabaya sana.
15. KWAMBA Meena alisikika akisema; hatuna ubaya na Nchimbi, tunampenda Nchimbi, hatuna ugomvi na Serikali, hatuna ugomvi na polisi! jamani mwenye mkanda na akausikilize vizuri. Sasa kama wanahabari hawakuwa na ugomvi na serikali maandamano ya nini? Kama wanahabari hawana matatizo na polisi je matamko na kulaani alikuwa analaaniwa nani na kwa nini? Kama wanahabari hawakuwa na tatizo na Nchimbi je kwa nini walimtimua? Mimi nina mashaka makubwa sana kuwa huyu Bw. Meena ndiye alimwalika Nchimbi.
16. KWAMBA nyie wahariri kupitia kwa katibu wenu mlikuwa mnajipendekeza kwa Nchimbi kwa nini? nyie wahariri mlikuwa mnajifanya wazuri kwa nchimbi eti wabaya ni wanahabari wanaomtimua nchimbi mlikuwa mmeahidiwa nini? Si bure, mpaka mkajitoa bila aibu vile kumtukuza nchimbi, serikali na polisi kupitia kwa Meena baada ya kutoa hotuba ya kulaani na kukerwa na serikali na polisi, hakukuwa bure kuna jambo. Mlimwahidi aje na mtampatia nafasi ya kuongea naye kwa kujua 2015 yaja kajiingiza kichwa kichwa na kaja kweli.
17. KWAMBA baada ya hotuba zile kabla hatujaondoka jangwani nilikaa jirani na wahariri fulani (nawakumbuka watatu, Jesse Kwayu wa Nipashe, Bakari Machumu wa The citizen na Dennis Msacky wa Mwananchi) na hapa Jesse kalikoroga kwa kuhoji “hivi Nchimbi hawezi kuelewa mahali pa kuhudhuria na wapi kutohudhuria?”
18. KWAMBA kwa mshangao wa wengi Dennis Msacky alijibu kwamba nchimbi kagain political capital! jibu hili lilipingwa na wote, Jesse, Bakari nakumbuka hata mimi nilipinga. tukajaribu kumwonyesha Msacky namna alivyoaibika Nchimbi na hakupata ujiko wowote huku yeye aking’ang’ana “ehe huoni yeye kafika hapa ni waziri pekee aliyekuja hii ni njema ni political capital”! hakuna aliyemsikiliza na sote kwa pamoja tulimbamiza hadi akakubali kuwa rafiki yake kachemka. nasikia Dennis ni rafiki yake kipenzi Dk. Nchimbi. nami nasema namtilia shaka sana Dennis kuwa naye alihusika kumwalika Nchimbi jangwani.
Kicheere, Tungi Kigamboni Tanganyika Territory
Uthibitisho:
mimi Nyaronyo Mwita Kicheere nathibitisha kwamba yote niliyoyasema hapo juu hasa aya ya 1 -18 ni kweli tupu na si kitu kingine bali ukweli mtupu.
Kicheere, Tungi Kigamboni Tanganyika territory
Ubaya ni kwamba ukweli huu unalifanya Jukwaa la Wahariri kuwa jukwaa la wanafiki hata kama si wote ni wanafiki. watu wako kwenye jukwaa kugain materially na politically. Yaani kujiweka katika good books of Government!!!!!!!!
CHANZO: Jukwaa la Mabadiliko