|
Na. Mwandishi Maalum
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge; Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb) ameuagiza uongozi wa Shirika la Tija la Taifa kuwa wabunifu katika utoaji wa elimu kwa umma ili jamii iweze kujua kazi na huduma zinazotolewa na shirika hilo.
Mhagama ametoa agizo hilo alipotembelea Shirika la Tija la Taifa (NIP) Januari 15,2016 kwa lengo la kujionea kazi zinazotekelezwa pamoja na changamoto zinazolikabili shirika hilo.
“Uongozi lazima uangalie changamoto zinazolikabili shirika hili na kuangalia namna ya kugeuza changamoto hizo kuwa fursa muhimu na kutoa elimu kwa umma wa Watanzania ili wajue umuhimu wa kutumia huduma yenu kwa lengo la kujiletea maendeleo,”alisema Mhagama
Waziri alielekeza kuwa lazima viongozi wa NIP wawe wabunifu katika kutumia vyombo mbalimbali vya habari vinavyoweza kuwafikia wananchi wa aina zote huku akisisitiza kuangalia vipindi ambavyo havihitaji kulipiwa.
“Nendeni mkaongee na wadau wa vyombo vya habari maana utakuta kuna fursa nyingi mngeweza kuzitumia bila gharama yoyote. kuna vipindi kama vile Kipindi cha Jambo Tanzania cha TBC 1, kipindi cha Kumekucha cha ITV, kipindi cha 360 Clouds Tv na Tuongee asubuhi cha Star Tv na vingine vingi amabavyo mnaweza kuvitumia kuwafikia wananchi wengi,” alisisitiza Mhe. Mhagama.
Waziri alisema kuwa kwa kutumia ubunifu na fursa zilizoko kwenye vyombo vya habari shirika litapata kujitangaza bila kutumia gharama na kuweza kuyafikia malengo kama kuboresha ujuzi na uelewa wa usimamizi wa rasilimaliwatu, kuchapisha na kusambaza fasihi na kuboresha utendaji wa Taasisi za umma na zisizokuwa za umma.
Wakati akimkaribisha waziri, Mkurugenzi Mtendaji wa NIP Bw.Novatus Massao alieleza kuwa miongoni mwa changamoto zinazokabili shirika hilo ni suala la taswira hasi kwa jamii na uelewa mdogo wa jamii kuhusu faida na umuhimu wa Shirika hilo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Bodi ya NIP, Prof.Samwel Wangwe aliahidi kuwa shirika hilo litahakikisha linatekeleza maagizo yote ya Mhe. Mhagama ili kuwezesha watanzania kuelewa na kutumia huduma za shirika hilo.
Aidha, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala Bw.Raphael Loishiye alimshukuru Mhe. Waziri kwa kufanya ziara katika Shirika hilo na kujionea mazingira na changamoto wanazokabiliana katika utekelezaji wa majukumu yao.