Mh Mbilinyi a.k.a mr ii Akabidhiwa Ofisi haina hata Kigoda


MBUNGE wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi, ameanza kukumbana na machungu ya uongozi baada ya kukabidhiwa ofisi ambayo haina samani ndani yake.

Ofisi hiyo imebainika kukosa samani zinazotakiwa baada ya mbunge huyo kwenda kwa Mkurugenzi wa Jiji, Juma Rashid Idd, kwa lengo la kukabidhiwa rasmi ili aanze kazi za kuwatumikia wananchi wa Jiji la Mbeya.

Makabidhiano hayo yalifanyika juzi, majira ya saa 3.30 kati ya Mkurugenzi wa Jiji Idd na mbunge huyo, lakini lilikwama kutokana na mazingira ya uchafu yaliyo mithili ya ofisi iliyotelekezwa na haikuwa na samani ndani yake.

Baadhi ya maofisa wa jiji la Mbeya ambao walishuhudia tukio la kukabidhiana ofisi, waliiambia Tanzania Daima Jumatano kuwa kutokana na kukosekana kwa samani katika ofisi hiyo, Mbunge huyo hakuweza kukabidhiwa hadi hapo zitakaponunuliwa nyingine.

“Ni kweli Mbunge kashindwa kukabidhiwa ofisi hiyo maana hali ya ofisi ni mbaya, ukiangalia kwa haraka utagundua kabisa kuwa jamaa…(akimaanisha mbunge aliyepita Benson Mpesya CCM) hakuwa akiitumia kwa muda mrefu,” alisema mmoja wa maafisa jiji ambaye aliomba jina lake lisitajwe.

Mbali ya kutokuwa na samani, ofisi hiyo pia haikuwa na mafaili yoyote yanayotumika kuhifadhia nyaraka mbalimbali za kiofisi ikiwemo mipango iliyotekelezwa na inayotarajia kutekelezwa na mbunge.

Kwa mujibu wa taratibu za Bunge, kila mwezi mbunge hupokea sh 500,000 kwa ajili ya shughuli za jimbo, ikiwemo ununuzi wa vifaa mbalimbali vya ofisi.

Habari na na Moses Ng’wat, wa Tanzania Daima