Mh. Kikwete in Malabo for AU Summit

Malabo, Equatorial Guinea

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Juni 30, 2011, alikuwa miongoni mwa viongozi wa Serikali na nchi 53 za Afrika walioshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa 17 wa Viongozi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ulioanza katika mji mkuu wa Equatorial Guinea wa Malabo.

Kabla ya ufunguzi rasmi wa mkutano huo wa siku mbili, viongozi hao wa nchi wanachama wa AU wameshiriki katika halfa ya kupanda miti kwenye bustani za ukumbi wa kisasa kabisa wa Palace of Conferences ulioko katika kijiji kipya na cha kisasa cha Sipopo, nje kidogo ya Malabo, katika Kisiwa cha Bioko, ambako mkutano huo unafanyika kwa kila kiongozi kupata mti katika nchi yenye misitu mingi na mikubwa ya eneo la Equator.

Kwenye sherehe hiyo ya ufunguzi wa Mkutano huo wa 17 wa viongozi wa AU, washiriki wamesimama kimya kwa dakika moja kwa kumbukumbu ya viongozi wawili wa Afrika ambao wamefariki dunia karibuni akiwamo Rais Frederick Chiluba, kiongozi wa zamani wa Zambia na rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mkutano huo wa 17 pia umewakaribisha kwa mara ya kwanza viongozi wapya wa baadhi ya nchi za Afrika akiwamo Rais Mamadou Yusuf wa Niger, Rais Alasane Quattara wa Ivory Coast na Mheshimiwa Iklilou Dhoinine wa Comoro ambao wameingia madarakani kufuatia chaguzi za kidemokrasia katika nchi zao.

Miongoni mwa viongozi ambao wamezungumza kwenye sherehe hiyo ya ufunguzi ni Meya wa Jiji la Malabo ambaye amewakaribisha wajumbe wa mkutano huo katika jiji la Malabo pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Afrika Mheshimiwa Jean Ping ambaye kwa ufupi ametoa ripoti ya mambo makuu yaliyofanywa na AU katika miezi sita iliyopita tokea kikao cha mwisho kilichofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, ambako ndiko makao makuu ya AU.

Viongozi wengine waliozungumza kwenye ufunguzi huo ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Mheshimiwa Asha Rose Migiro, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu wa Arab League na Mwenyeji wa mkutano huo Rais Theodoro Obing Nguema Mbagoso.

Mheshimiwa Ping pia amesema kuwa mageuzi ambayo dunia imeyashudia katika baadhi ya mataifa ya Afrika Kaskazini ni ushahidi wa kutosha kwa Afrika inahitaji kuongeza kasi yake ya mageuzi na utekelezaji wa demokrasia kama kama inavyodaiwa na mazingira ya sasa ya Afrika na yale ya dunia.

Rais Kikwete na ujumbe wake ambao unamshirikisha Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete aliwasili mjini Malabo usiku wa jana tayari kushiriki katika mkutano huo ambao mada kuu yake itakuwa “Jinsi ya Kuharakisha Uwezeshaji wa Vijana kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu.”

Rais Kikwete alitarajiwa baadaye leo jioni kuzungumza katika kikao cha kujadili mada kuu ya mkutano huo kufuatia ufunguzi uliofanywa na Mwenyekiti wa sasa wa AU ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Equatorial Guinea, Mheshimiwa Theodoro Obiang Nguema Mbasogo.

Mbali na kushiriki katika mkutano huo muhimu, Rais Kikwete pia ataendesha mkutano wa viongozi wa Afrika katika kupambana na ugonjwa wa malaria wa ALMA (African Leaders Malaria Alliance katika nafasi yake kama mwenyekiti wa kwanza wa umoja huo wa wakuu wa nchi za Afrika katika kupambana na ugonjwa wa malaria.

Rais Kikwete pia atapata nafasi ya kukutana na watu mbali kujadili masuala yanayohusu Tanzania akiwamo Mheshimiwa Andrew Mitchel, Waziri wa Misaada ya Kimataifa ya Maendeleo wa Uingereza na Mheshimiwa Antonio Guterres, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR).

Baadaye leo jioni, Rais Kikwete atajiunga na viongozi wake wengine wa Afrika kwenye halfa ya chakula cha jioni iliyoandaliwa kwa ajili ya viongozi hao wa Afrika na mwenyeji wao, Mheshimiwa Theodoro Obiang Nguema Mbasogo.

Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,

Safarini,

Malabo, Equatorial Guinea.

01 Julai, 2011