HALI ya Mgonjwa wa Ebola aliyegundulika hivi karibuni nchini Marekani inaendelea kuwa mbaya huku madaktari wanaomtibu wakihaha kutafuta dozi za kumwanzishia mgonjwa huyo. Thomas Eric Duncan ambaye ni mgonjwa pekee wa Ebola nchini Marekani aliyegundulika kuugua ugonjwa huo hali yake inazidi kuwa mbaya huku kukiwa hakuna vidonge vya dawa za majaribio ambavyo yasemekana vinaweza kupambana na virus vya ugonjwa huo.
Eric Duncan ambaye aliwasili Jijini Texas wiki tatu zilizopita akitokea nchini Liberia amegundulika kuugua ugonjwa huo na tayari ametengwa huku akipatiwa huduma maalum kuepusha kusambaza virus vya ugonjwa huo kwa raia wengine wa nchi hiyo.
“Mgonjwa huyu pekee wa Ebola bado anapatiwa huduma maalum jijini Dallas, japokuwa hali yake ni mbaya kwa sasa,” alisema kwa waandishi wa habari jana Mkurugenzi wa Kituo cha Udhibiti na Ushughulikiaji wa Magonjwa nchini Marekani, Dk. Thomas Frieden akizungumza na wanahabari.
Aidha alisema kwa sasa hawana dozi yoyote ya dawa ambayo wangepaswa kumwanzishia mgonjwa huyo (ZMapp) kwa kuwa zilipelekwa maeneo ya ugonjwa baadhi ya mataifa ya Afrika Magharibi ambayo yameshambuliwa zaidi na Ebola. Alisema wameshindwa kumuanzishia hata vidonge vingine vya majaribio kwa kuwa havipo tayari kuanza kutumiwa kwa wagonjwa, japokuwa familia ya mgonjwa Eric Duncan wameomba apewe hivyo hivyo.
Hata hivyo, Dk. Thomas Frieden alisema ofisi yake inajiandaa kumpa taarifa ya hali halisi ya ugonjwa huo nchini Marekani, Rais Barack Obama leo (Jumatatu). Ugonjwa wa Ebola tangu uibuke Machi, 2014 tayari unasemekana kuua watu 3400 kati ya wagonjwa wanaokaribia 7500 walioshukiwa kupatikana na virusi vya ugonjwa husika.
-Reuters