Mgomo wa madaktari wawatesa wagonjwa Dar

Jengo la Wodi ya Wazazi Muhimbili

Na Mwandishi Wetu

MGOMO wa madaktari nchini uliendelea jana jijini Dar es Salaam huku wananchi wakilalamikia ukosefu wa huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali hivyo kuiomba Serikali kumalizia mgogoro huo wa wataalamu wa afya unaoshinikiza kujiuzulu kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda na Naibu wake Dk. Lucy Nkya.

Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Thehabari imeshuhudia wagonjwa wakisubiri kupatiwa huduma bila mafanikio na wengine wakilalamikia hali hiyo kwa kile wanachoeleza kuwa wametoka mbali ya jiji la Dar es Salaam.

Baadhi ya wagonjwa wameueleza mtandao huu kuwa tangu wamefika hospitalini hapo hawajapata huduma yoyote, huku wengine wakidai kuwa wamepangiwa tarehe za mbali hali inayowapa wasiwasi wa mustakabali wa afya zao.

Katika kitengo cha Taasisi ya Mifupa (MOI) wagonjwa wamelalamika kutokuwepo kwa huduma katika taasisi hiyo, huku Msemaji wa MOI, Almas Jumaa akisema huduma za wagonjwa wa nje zimesimamishwa kutokana na madaktari kugoma.

Jumaa amesema kati ya madaktari zaidi ya 70 wanaotoa huduma katika taasisi hiyo ni madaktari 15 tu, wanaoendelea na kazi. Mgomo huo wa madaktari umeanza jana licha ya serikali kuwasihi kutogoma kwa kile ilichoeleza kuwa madai yao yanashughulikiwa.