JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni linamshikilia Katibu wa Ummoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (UWAMATA), Mboka Ambokile kwa tuhuma za kuhamasisha mgomo ambao ulisabisha abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani cha Ubungo (UBT) jijini Dar es Salaam jana kushindwa kuondoka kwa wakati hadi polisi walipoingilia kati.
Mgomo huo umekuja baada ya wamiliki wa mabasi hayo kupinga uamuzi wa serikali kupunguza uzito unaotakiwa kwenye mabasi na malori pindi yanapopimwa kwenye mizani. Ambapo awali uzito wa mabasi ulitakiwa kutovuka kilo 8,400 mbele na kilo 10,500 huku kwa magari ya mizigo kilo 18,000 kwa mbele na nyuma kilo 25,200, kiasi ambacho kwa sasa kimepunguzwa kwa malori hadi kufikia uzito wa kilo 17,000 kwa mbele na kilo 24,000 kwa nyuma.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ambokile alisema anashangazwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kumkamata yeye kwa madai kwamba ndio chanzo cha mgomo ilhali mgomo ulikuwa wa wamiliki wa mabasi na wala si madereva. “Binafsi naona sijui tuseme ni uelewa mdogo wa mambo kwa askari wetu…mgomo haukuwa wa kwetu (Chama cha Madereva) ni kati ya wamiliki na Serikali sasa hapo mimi nahusikaje?,” alisema Ambokile.
Alisema walichokifanya askari ni kuamua kumdhalilisha yeye kitendo ambacho si cha ungwana bali ni mabavu. “Tunakaa na wanasheria wetu tuangalie nini cha kufanya baada ya kunifanyia tukio hilo. Alisema askari wa kutuliza ghasia FFU walimkamata na kumfunga pingu kisha kumpeleka hadi Kituo cha Polisi Oysterbay na kuhojiwa kwa muda kisha baadaye kuachiwa.
Hata hivyo madai mengine ya wamiliki wa mabasi ni kupinga mabasi kupimwa uzito kwenye vituo vya mizani kitendo ambacho Serikali kupitia kwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli imekipinga na kuelekeza mabasi yote yatapimwa na kufuata uzito ulioelekezwa kwe sheria.
Mmoja wa wadau wa usafirishaji aliyejitambulisha kwa jina la Abdulrazek Arosto alisema kumekuwa na tofauti za uzito kati ya mzani mmoja hadi mwingine na hali hiyo inasababishwa na mabasi mengi yanayotumika nchini kutokuwa na mfumo mmoja wa muundo wa chesesi ambazo pia zina uzito tofauti. “Hii ni changamono kwani Serikali inapaswa kuangalia muundo wa magari haya ya abiria tofauti na ilivyo sasa, magari yanayotumika yana miundo tofauti, mengine yana gia zaidi ya saba wakati kiusahihi inatakiwa kuwa na gia sita…hali hii ndio inayoleta hata utofauti mkubwa kiuzito kutoka muundo mmoja hadi mwingine,” alifafanua Arosto.
Wakati huo huo Chama cha Kutetea Abiria (CHAKUA), kimelaani kitendo cha wamiliki wa mabasi kuwatumia abiria kama fimbo ya kuikomoa Serikali dhidi ya mgogoro wa uzito wa magari unaoendelea. Akizungumzia suala hilo, Katibu wa CHAKUA, Bwana Gelvas alisema kitendo cha wamiliki kukubali kukatisha tiketi kwa abiria na baadaye kugoma ni kuvunja makubaliano kati yao na abiria.
“Abiria wameingia mkataba kati yao na wamiliki kwamba wasafirishwe hadi wanapo kwenda sasa kitendo cha mmiliki kugoma ilhali amekatisha tiketi ni kinyume na makubaliano na hali hiyo inatakiwa ashtakiwe…sisi tunaomba sana hawa wamiliki wasimtumie abiria kama fimbo kuiadhibu Serikali huu sio ungwana,” alisema Gelvas.
Mgomo huo ulioanza majira ya asubuhi ulimalizika majira ya saa nne baada ya wamiliki kukubaliana na Jeshi la Polisi kwamba waendelee kutoa huduma wakati suala hilo likifanyiwa kazi kwa mazungumzo ya pande zote. Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga alisema kikosi chake kimejipanga kuhakikisha mabasi yaliyochelewa yanasafiri kwa usalama huku yakifuata sheria za usalama barabarani.
Alisema mabasi yatakayochelewa kufika hayata ruhusiwa kusafiri usiku baada ya muda wa kawaida kupita, hivyo yatazuiliwa na kuruhusiwa kuondoka siku inayofuata ili kulinda usalama wa abiria na mali zao.
Serikali