Na Mwandishi Wetu,Mbeya
KESI ya kijinai inayomkabili mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mbeya Mjini, Sambwee Shitambala, imeendelea kusikilizwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Mbeya.
Shitambala ambaye ni Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, anatuhumiwa kwa kosa la kuvamia eneo linalodaiwa simali yake na kujenga kwenye eneo la kiwanja hicho mali ya mtu mwingine kinyume na sheria katika kiwanja kilichopo Gombe Jijini hapa. Kosa hilo ni kinyume cha sheria ya 266(a) sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 .
Akisomewa shitaka hilo na Mwendesha mashitaka wa serikali, Wakili Baraka Mgaya, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Girbelt Ndeuluo, alidai mtuhumiwa alitenda kosa hilo kati ya Juni, 2012 na February 2013 katika eneo la Gombe lililopo Jijini Mbeya.
Alidai kuwa mtuhumiwa aliingia kwenye eneo la ardhi kiwanja namba 27 na 28 kilichopo katika eneo la Block Bb kata ya Itezi Jijini hapa,mali ya Jaswinda Palsin(Singa Singa) ambaye ni raia kutoka bara la Asia na kujenga nyumba yake ya makazi kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumfanyia maudhi raia huyo.
Hakimu Ndeuro, aliihairisha kesi hiyo hadi Septemba 15, mwaka huu, ambapo upande wa mashitaka utakapoleta watuhumiwa wengine wanne watakaoungana na Shitambala kujibu tuhuma zinazowakabili za kuingia kwa jinai kwenye eneo la kiwanja cha Singa Singa huyo.