Na Mtua Salira EANA Arusha
MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) yenye makao yake Makuu Mjini Arusha, Tanzania imeanza kusikiliza kesi ya mgogoro wa ardhi kati ya serikali ya Kenya na kabila dogo la wawindaji la Ogiek juu madai yao ya haki ya ardhi.
Mahakama hiyo inayoketi kwa muda mjini Addis Ababa, Ethiopia inasikiliza madai ya jamii hiyo inayoishi msituni dhidi ya serikali ya Kenya kwa kukiuka na kuwanyima haki ya kumiliki ardhi, linaripoti Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA).
Katika taarifa yake ya ufunguzi wa kesi hiyo Alhamisi, Kamishina wa Haki za Binadamu Afrika, Pacifique Manirakaza alidai mahakamani kwamba serikali ya Kenya imekiuka haki mbalimbali ya jamii ya Ogiek ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi, kumiliki mali, rasilimali asilia, maendeleo, dini na utamaduni.
“Mlalamikiwa (serikali) amekuwa kwa muda wa miaka mingi akifanya mfululizo wa vitendo vya ukiukwaji wa haki kama vile kuwabughudhi na kuwaondoa maeneo wanayoishi Wagiek bila kuwasiliana nao kwanza au kuwalipa fidia kutoka kwenye Msitu wa Mau, ambao ni eneo la asili yao, ambako wamekuwa wakiishi kwa miaka mingi tangu enzi za mababu zao na ni eneo muhimu sana kwa maisha yao kama wakazi wa eneo la asili,” alieleza Manirakaza, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Ottawa, Kitivo cha Sheria.
Hii ni mara ya kwanza kwa mahakama hiyo iliyoanza shughuli zake mwaka 2006, kusikiliza kesi inayohusu haki za kabila dogo katika kesi ya kwanza ya aina hii. Awali kesi hiyo iliwasilishwa mbele ya Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu lakini ikapelekwa kwenye mahakama hiyo kwa misingi kwamba malalamiko hayo ni mazito na yanagusa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Wakili Kiongozi wa mlalamikaji, Tom Nyanduga alisema kwamba kesi hiyo ni mfano wa jamii ambayo haina uwezo lakini imeamua kupigania haki zao bila kujali itawachukua muda gani. Kiasili kabila la Ogiek ni warina asali na wanaishi kwa kutegemea matunda ya porini, mizizi, uwindaji wanyamapori na ufugaji nyuki wa jadi.
Katika kesi hiyo serikali ya Kenya imewakilishwa na timu ya mawakili watatu ikiongozwa na Muthoni Kimani, Naibu Mwanasheria Mkuu ambaye alikana madai yote na kusema kwamba Kenya ina hamu ya kujenga nchi ya kisasa na kuhakikisha kwamba raia wake wote wanaishi maisha bora bila ubaguzi wowote. Ameiomba mahakama hiyo isiipokee kesi hiyo na badala yake iirejeshi Kenya ili iweze kupatiwa suluhisho.
Mashahidi wawili walisikilizwa siku hiyo ya ufunguzi wa kesi iliyokuwa inasikilizwa na jopo la majaji tisa lililokuwa linaongozwa na Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Augustino Ramadhani kutoka Tanzania.