Mgodi wa Bulyanhulu wachangia mil. 150 ujenzi wa shule, zahanati

Nembo ya Kampuni ya Barrick

Na Mwandishi Wetu

Kahama

MGODI wa dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold (ABG) mwezi huu umechangia karibu sh. milioni 150 kwenye miradi ya elimu na afya iliyopo katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga, mgodi huo umesema katika taarifa yake leo.

Migodi minne inayomilikiwa na kampuni ya ABG nchini Tanzania — Bulyanhulu, North Mara, Tulawaka na Buzwagi — imetumia mabilioni ya shilingi kwa miaka kadhaa sasa ili kuwekeza kwenye miradi ya elimu, afya, maji na miundombinu, yenye lengo ya kuboresha maisha ya wanakijiji wanaoishi karibu na migodi hiyo.

Katika mchango wake wa hivi karibuni, mgodi wa Bulyanhulu (BGML) ulitoa mchango wa fedha wa zaidi ya shilingi 86.4 milioni kwa kijiji cha Kakola kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na madarasa matatu kwenye shule.

Kakola, ambacho ni kijiji cha karibu zaidi kuliko vyote na mgodi huo, kimenufaika na misaada mbalimbali kutoka ABG kwa miaka mingi na kujenga uhusiano wa karibu baina ya wanakijiji na mgodi huo.

Akizungumza katika utiaji wa saini wa makubaliano ya msaada huo, kaimu meneja wa mahusiano ya jamii wa mgodi wa BGML, Theophilo Tweve, alisema kuwa mgodi umechangia 42,707,750/- kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na 43,702,350/- nyingine kwa ujenzi wa madarasa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kakola, Emmanuel Bombeda, ameushukuru mgodi huo kwa misaada yake ya mara kwa mara kwa wananchi wa eneo hilo na kuahidi kusimamia matumizi sahihi ya misaada hiyo ili kuboresha hali ya maisha ya wanakijiji.

Pia aliupongeza mgodi huo kwa msaada wake wa awali kwenye kuchimba visima kadhaa ambavyo vimeweza kutokomeza tatizo sugu la muda mrefu la kukosekana kwa maji safi na salama kwenye eneo hilo.

Wakati huo huo, Meneja Mkuu wa mgodi wa BGML, Dennis Hoof, na viongozi wengine wa mgodi huo Novemba 3 mwaka huu walitembelea mradi wa ujenzi wa shule ya Kiislamu inayojengwa karibu na mgodi.

Ujenzi wa shule hiyo unagharamiwa kwa michango ya hiari inayotolewa na wafanyakazi Waislamu na wasio Waislamu wa mgodi wa Bulyanhulu kupitia kwa makato ya kila mwezi kutoka kwenye mishahara yao.

Mradi huo wa elimu mpaka sasa umegharimu jumla ya 62,757,000/-, huku madarasa mawili na chumba cha ofisi ya walimu vikiwa tayari vimeshajengwa.

Moja ya madarasa linatumiwa kwa wanafunzi wa vidudu wakati darasa jingine linatumiwa na wanafunzi wa darasa la kwanza lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 45.

Meneja Mkuu wa mgodi, Dennis Hoof, aliwapongeza waanzilishi wa shule hiyo kwa kuja na mradi huo wenye lengo la kuinua elimu kwenye eneo hilo.

Aliahidi kuwa wafanyakazi wa mgodi huo wataendelea kutoa michango yao kuhakikisha ujenzi wa shule unakamilika.

Kampuni ya African Barrick Gold (ABG) ilitangaza Septemba mwaka huu uzinduzi wa Mfuko wa Maendeleo ambao utapewa fungu la dola za Marekani milioni 10 kila mwaka ili kuendeleza miradi ya maendeleo ya jamii hapa nchini.

Fedha hizi ni nyingi kuliko zinazotolewa na makampuni yote nchini katika kutoa michango na misaada ya miradi ya maendeleo ya jamii.