Mgawo wa umeme wakwamisha kesi ya Lema

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA)

Na Janeth Mushi, Arusha

MGAWO wa umeme unaoyakabili maeneo anuai nchini, leo umeathiri kuanza usikilizwaji wa awali wa kesi inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) ya kupinga matokeo ya ubunge, inayosikilizwa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, baada ya mawakili wa upande wa wadai kushindwa kuwasilisha muhtasari wa shauri hilo.

Wapiga kura Musa Nkanga, Agness Mollel na Happy Kivuyo wa Jimbo la Arusha Mjini ndiyo waliofungua kesi hiyo ambayo iliahirishwa juzi baada ya Jaji Aloyce Mujulizi kutupilia mbali pingamizi zilizotolewa na mawakili wa Upande wa Wadaiwa. Leo kesi hiyo ilitakiwa kuanza kusikilizwa jambo ambalo lilishindikana. Wakili wa Upande wa wadai, Alute Mughwai aliieleza mahakama kuwa ameshindwa kuandaa muhtasari kwa kile baada ya umeme kukatika.

“Kwa bahati mbaya hatukuweza kutayarisha muhtasari wa kesi hii, kwa sababu ya tatizo la umeme, Jenereta ninayo lakini nayo kwa bahati mbaya ilikuwa imeisha mafuta na nilipokwenda wka wakili mwenzangu Modest Akida umeme nako ulikuwa umekatika,” alisema Alute.

Mughwai alisema kuwa kutokana na tatizo hilo la umeme, leo asubuhi
ndiyo wametayarisha muhtasari huo lakini wameshindwa kuwasilisha nakala yake kwa Wakili wa mdaiwa wa kwanza Method Kimomogolo na wakili Timon Vitalisa anayemtetea Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kwa mahakama hiyo.

Mbele ya Jaji anayesikiliza kesi hiyo Mujulizi, Alute aliiomba
mahakama hiyo kwa sababu shauri hilo linatakiwa kufuata utaratibu hivyo usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo uahirishwe ili mawakili wa upande wa wadaiwa nao waweze kupata muda wa kupitia Muhtasari huo, hadi Oktoba 17 mwaka huu.

Mughwai alidai kuwa katika Mahakama ya Rufaa, Octoba 7 na Octoba 11
anazo kesi katika mahakama hiyo ambazo nazo anazohitaji muda wa
kuzitayarisha. Kwa upande wake Wakili anayemtetea Lema, Method Kimomogolo alikubaliana ana ombi lililotolewa na Wakili wa Wadai na kudai kuwa watapata muda wa kutosha kupitia Muhtasari watakaopewa.

Kimomogolo aliiomba mahakama hiyo kuwa kutokana na kuahirishwa kwa
kesi hiyo wanaomba mahakama hiyo iweze kuwapatia nakala ya taarifa
alizoandika Jaji Mujulizi kwenye usikilizaji wa pingamizi na uamuzi wa
pingamizi hizo ili ziweze kuwaongoza katika mwenendo mzima wa shauri
hilo ili wasijikanganye kisheria.

Naye Wakili anayemtetea Mwanasheia Mkuu wa Serikali, Timon Vitalis
aliiomba Mahakama hiyo kumwelekeza Msajili wa Mahakama chini ya
kifungu cha 15 kifungu kidogo cha 2 Kanuni za Mwenendo wa uendeshaji
wa shauri za uchaguzi, kutoa taarifa ya tarehe muda na mahali ambapo
shauri hilo litasikilizwa.

Baada ya Hoja za pande zote mbili kuwasilishwa Jaji Mujulizi alisema
kuwa kwa kuzingatia Kikao cha Mahakama Kuu ya Rufani nchini
kinachoendelea mjini hapa hadi Octoba 13 mwaka huu, aliahirisha kesi
hiyo hadi Oktoba 17 mwaka huu saa 3 asubuhi.

Mujulizi alimwagiza Msajili wa wilaya kutekeleza kanuni za Mwenendo wa
uendeshaji wa shauri za uchaguzi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa muda, tarehe za kesi hiyo kusikilizwa na kumtaka aanzishe mchakato wa kuomba kuongezwa muda wa usikilizwaji wa kesi hiyo kwa madai kuwa muda uliobaki kusikilizwa kwa shauri hilo hautoshi.

Aidha Jaji huyo alimwagiza msajili huyo kutoa Nakala za taarifa alizoandika Jaji Mujulizi kwenye usikilizaji wa pingamizi na uamuzi wa
pingamizi kwa ajili ya Mawakili wa upande wa wadaiwa. Juzi Jaji huyo alisema Mahakama hiyo imetupilia mbali hoja zilizotolewa na Mawakili hao kutokana ana hoja hizo kutokukidhi vigezo kisheria na badala yake vimelenga katika mambo yasiyoijikita katika kesi hiyo.