Mganga anyofoa sehemu za siri za mteja wake na kutoweka

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Said Mwema.

Na Mwandishi Wetu, Urambo

MWANAMKE mmoja (66) mkazi wa Kijiji cha Mwendakulima Wilaya ya Urambo mkoani Tabora amefariki dunia baada ya mganga wa kienyeji kumnyofoa sehemu yake ya siri na kisha kukimbia nayo, alipokuwa akipatiwa matibabu kwa mganga huyo.

Marehemu huyo, Salome Shikombe jina tunalihifadhi kimaadili ya taaluma hii, alikwenda nyumbani kwa mganga, Kabula Mateo kutibiwa, ambapo hata hivyo haikuweza kujulikana mara moja ugonjwa gani ulikuwa unamsumbua marehemu huyo hadi kupatwa na kakasa huo.

Tukio hilo lilitokea Julai 6 mwaka huu, majira ya saa moja jioni Kijiji cha Mwendakulima, Urambo ambapo mganga huyo alimdanganya mgojwa wake kwamba ni lazima amchanje chale sehemu za mwili wake ili apone, kwani alikuwa amelogwa na wachawi, ghafla alimfyeka uke wake na kisha kukimbia nao na kwenda kusiko julikana.

Habari za uhakika kutoka Urambo na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Liberatus Barow zinaeleza kwamba marehemu alifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi baada ya kukatwa na mganga huyo katika sehemu zake nyeti, kwa madai kuwa anamkata ili aweze kupona ugonjwa unaomsumbua kwa muda mrefu.

Hata hivyo Kamanda wa jeshi la polisi mkoani hapa aliliambia gazeti hili kuwa juhudi za kumsaka mganga huyo zinaendelea na kwamba polisi wanamsaka hadi akamatwe ili afikishwe katika vyombo vya sheria na viweze kuchukua mkondo wake kwa tuhuma zinazo mkabili za kusababisha mauaji.

Alieleza kwamba uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mauaji hayo yanahusishwa na imani za kishirikina ambapo aliahidi kuwasaka waganga wote wenye tabia kama hiyo ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani, lengo ni kutokomeza kabisa vitendo hivyo vya kinyama kwa jamii.

Kamanda Barow ametoa wito kwa wananchi mkoani Tabora kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi juu ya watu kama hao, ambao wanajifanya kuwa ni waganga wa kienyeji kumbe ni mtapeli ambao wanaharaka ya kujipatia utajiri wa haraka.