Mfumuko wa Bei Wapanda Tanzania

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwim, Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Agosti, 2014 jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwim, Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Agosti, 2014 jijini Dar es Salaam.

Na Aron Msigwa – Maelezo, Dar es Salaam

MFUMUKO wa Bei wa Taifa kwa mwezi Agosti, 2014 umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 6.5 iliyokuwepo mwezi Julai kutokana na kuendelea kupanda kwa bei ya baadhi ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo akitoa taarifa ya ongezeko hilo Dar es Salaam, alisema kuwa bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo Bia, Sare za shule, mkaa, samani za nyumbani na bidhaa za vitambaa kwa matumizi ya nyumbani zimechangia kuwepo kwa ongezeko dogo la mfumuko wa bei nchini.

Ameongeza kuwa kuwepo kwa ongezeko la gharama kwenye huduma ya meno, huduma za vyakula kwenye migahawa na zile za kulala hotelini katika maeneo mbalimbali nchini pia zime kumechangia mfumuko wa bei. Aidha, Kwesigabo amebainisha kuwa kuongezeka kwa Fahirisi za bei kwa maana ya kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma mbalimbali zinazotumiwa na sampuli wakilishi ya kaya binafsi nchini hadi 149.31 kwa mwezi Agosti 2014 kutoka 149.16 za mwezi Julai kumechangiwa na kupanda kwa gharama ya bidhaa zisizo za vyakula.

Kuhusu mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi kwa mwezi Agosti alisema kuwa umeongezeka kwa asilimia 0.1 huku uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi Agosti, 2014 ukipungua na kufikia shilingi 66 na senti 97.

“Kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali kuna athari kwa fedha yetu, hii inamaanisha kwamba, uwezo wa fedha yetu katika kununua huduma na bidhaa za mlaji unapungua, mfumuko wa bei unapopanda thamani ya shilingi nayo inashuka,”

Kwa upande wa ulinganifu wa mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, Kwesigabo ameeleza kuwa una mwelekeo unaofanana na kuongeza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya kwa mwezi Agosti umefikia asilimia 8.36 ikilinganishwa na 7.67 za mwezi Julai huku Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 2.8 mwezi Agosti ikilinganishwa na asilimia 4.3 za mwezi Julai.