Mfumuko wa Bei Nchini Tanzania Wazidi Kuongezeka

Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraim Kwesigabo  akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu  mfumuko wa bei nchini.

Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraim Kwesigabo
akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu  mfumuko wa bei nchini.

Na Aron Msigwa – MAELEZO
 
OFISI ya Taifa ya Takwimu imeeleza kuwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Aprili umeongezeka ikilinganishwa na mwezi uliopita kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma mbalimbali. Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na sensa ya Watu na Makazi, Ephraim Kwesigabo amesema kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Aprili 2014 umeongezeka na kufikia asilimia 6.3 kutoka asilimia 6.1 za mwezi uliopita.
 
Alisema kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma mbalimbali kwa mwezi Aprili 2014 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na ile iliyokuwepo mwezi Machi huku kukiwa na ongezeko dogo la upandaji wa bei kwenye baadhi ya bidhaa na huduma kwa mwezi huu ikilinganishwa na bei za mwezi uliopita. Alisema kuwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na migahawa kwa mwezi Aprili umeongezeka hadi

asilimia 8.5 kutoka asilimia 7.9 za mwezi Machi mwaka huu na kuongeza kuwa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi imeongezeka hadi asilimia 7.8 kutoka asilimia 7.2 za mwezi uliopita huku badiliko la fahirisi za bidhaa zisizo za vyakula likipungua hadi asilimia 4.9 kwa mwezi Aprili 2014 kutoka asilimia 7.2 iliyokuwepo mwezi uliopita.
  
Kwa upande wa  mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi, amefafanua kuwa kumekuwa na ongezeko dogo la asilimia 0.7 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 0.6 kwa lililokuwepo mwezi Machi mwaka huu, huku fahirisi za bei za taifa zikiongezeka hadi kufikia 150.50 kwa mwezi Aprili 2014 kutoka 149.49 za mwezi Machi.
 
Amezitaja bidhaa zilizochangia ongezeko la fahirisi za bei nchini kuwa ni pamoja na mchele, mahindi, unga wa Muhogo, Kuku wa kienyeji, dagaa, samaki wakavu, matunda, karanga na mihogo. Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia ongezeko la fahirisi amesema ni pamoja mkaa wa kupikia, huduma za matibabu, mafuta ya dizeli na gharama ya kusaga nafaka. Kuhusu uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma kwa mwezi Aprili Bw. Kwesigabo amesema kuwa umepungua na kufikia shilingi 66 na senti 45.
 
“Kupungua kwa thamani ya Shilingi kunamaanisha kwamba, kama mtu alikuwa na uwezo wa kununua bidhaa kwa Shilingi 100 kwa mwaka jana, kwa kipindi hiki itampasa aongeze zaidi ili aweze kununua kitu kama kile kile mfano badala ya shilingi 100 inabidi atumie shilingi 134,”
 
Kuhusu ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya umeongezeka na kufikia asilimia 6.41 kwa mwezi Aprili 2014 kutoka asilimia 6.27 za mwezi Machi, huku Uganda ikiwa na mfumuko wa asilimia 6.7 kwa mwezi huu ikilinganishwa na 7.1 za mwezi uliopita.