Mfuko wa Hiari wa PSPF Wanufaisha Wakazi wa Ukonga
Na: Genofeva Matemu – Maelezo
Wananchi zaidi ya 500 kutoka zoni ya ukonga jijini Dar es Salaam wamejitokeza na kujisajiri kuwa wanachama wa hiari katika mfuko wa hiari wa PSPF ili kuweza kunufaika na mafao yatolewayo na mfuko huo.
Wananchi hao walipata fursa ya kujisajiri wakati wa semina ya ujasiriamali iliyofanyika siku ya jana maeneo ya Ukonga jijini Dar es Salaam na kuudhuriwa na wananchi wapatao 1600 kutoka zoni ya Ukonga na maeneo mengine ya jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani.
Akizungumza wakati wa semina hiyo Afisa Uendeshaji kutoka Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) Bw. Delphin Richard amesema kuwa mfuko wa hiari wa PSPF uliundwa kwa ajili ya kutoa fursa kwa wananchi kuwa na akiba ya ziada kwa kutoa uhuru kwa mwanachama kuchangia kwa kutegemea upatikanaji wa kipato cha ziada kitakachomwezesha kujiwekea akiba.
Bw. Richard amesema kuwa lengo la PSPF ni kushiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii ili kuweza kutoa elimu ya mfuko wa hiari wa PSPF hivyo kutoa nafasi kwa wajasiriamali, wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, na watu binafsikuchangia katika mfuko wa hiari kipato chao cha ziada kwa ajili ya akiba ya ziada.
Kwa upande wake Afisa Masoko Bibi. Sarah Adebe amesema kuwa jamii imekua na muitikio mkubwa wa kujisajiri katika mfuko wa hiari wa PSPF kwani mfuko huo unatoa huduma kwa kuchangia gharama ndogo hivyo kuwanufaisha wanachama hasa wa kipato cha chini.
Naye Mjasiriamali kutoka zoni ya Ukonga Bi. Doris Kimaro amesema kuwa ujio wa elimu ya mfuko wa hiari wa PSPF ni mafanikio makubwa katika familia yake kwani atatumia nafasi aliyoipata kwa kuchangia kipato chake cha ziada ili aweze kunufaika na fao la elimu litakalomuwezesha kukidhi mahitaji yake ya baadae.
Mfuko wa hiari wa PSPF umelenga kusaidia jamii kwa kuwa na mafao saba ambayo ni fao la elimu, fao la ujasiriamali, fao la uzeeni, fao la kifo, fao la ugonjwa/ulemavu, fao la kujitoa na fao la matibabu.