Na Mwandishi Wetu
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeanza kufanya zoezi la ukaguzi na uhakiki wa vitambulisho vya matibabu kwa wanachama wake kazia ambayo itafanyika kwa nchi nzima.
Akitoa taarifa leo kwa vyombo vya habari Makao Makuu ya Mfuko huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emmanuel Humba amesema ukaguzi utafanyika katika vituo vya ngazi zote vya matibabu kwa lengo la kubaini uhalali wa vitambulisho hivyo.
Humba amesema kuwa lengo la ukaguzi huo ni kutaka kubaini uhalali wa vitambulisho vya matibabu lakini pia matumizi yake katika vituo vya kutolea matibabu. Amesema hatua hio imefikiwa baada ya uongozi wa mfuko kubaini matumizi yasiyo halali ya vitambulisho hivyo yanayofanywa na baadhi ya wanachama wasio waaminifu.
“Uongozi umebaini uwepo wa wanachama ambao wamepoteza vitambulisho vyao ambavyo vinatumiwa na watu wengine walioviokota, hivyo kusababisha mfuko kuingia gharama za matibabu kwa watu wasio wanachama wa mfuko,” alisema Humba.
Aidha ameongeza kuwa mfuko umebaini udanganyifu mwingine unaofanywa na wanachama wa kuazimana vitambulisho vya matibabu jambo ambalo liko kinyume na taratibu za mfuko. Udanganyifu mwingine ni ule wa baadhi ya wanachama kutoa nakala vitambulisho hivyo kwa kisingizio cha kutaka visichakae hali inayosababisha udanganyifu mkubwa katika matibabu.
“Sababu nyingine ya ukaguzi wa vitambulisho inatokana na wastaafu kutorejesha vitambulisho vya matibabu na vya wategemezi wao baada ya kustaafu utumishi wa umma. Utaratibu wa Mfuko, unamtaka mstaafu kurejesha kitambulisho chake na vya wategemezi wake ili aweze kupewa kitambulisho kingine kwa ajili yake na mwenza wake.”
Pamoja na hayo amesema zoezi hilo pia litabaini watumishi wanaoendelea kuhodhi vitambulisho vya matibabu wakati wakiwa wameacha kazi ama kuachishwa kazi hivyo kutochangia, wanatakiwa kuvirejesha wakati zoezi la uhakiki linaendelea.
Akifafanua zaidi alisema ukaguzi huo mbali na mafanikio mengine, utausaidia mfuko kuziba mianya ya udanganyifu katika huduma za matibabu zinazotolewa na mfuko lakini pia kuhakikisha kuwa ni wanachama peke yao ndio wananufaika na matibabu hayo.
“Kutokana na hali hiyo, Mfuko unawaomba wanachama wote kuwa walinzi wa huduma za matibabu na si kuwa chanzo cha tatizo la udanganyifu katika matibabu. Mfuko pia unawaomba wanachama na wananchi kwa ujumla kushirikiana na mfuko katika hali na mali kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kufanyika udanganyifu wa aina yoyote dhidi ya mfuko,” alisisitiza mkurugenzi huyo.
Hata hivyo amesema kwa wanachama waliopoteza vitambulisho wanatakiwa kufuata taratibu zilizowekwa na mfuko kwa ajili ya kupata kitamabulisho kingine na si kufanya udanganyifu wowote. Mfuko hautasita kuchukua hatua kali kwa watakaobainika na matumizi ya udanganyifu ya vitambulisho vya matibabu kwa kuwa yanasababisha hasara kubwa kwa Mfuko.
“Kwa wanachama na wananchi watakaobaini udanganyifu wasisite kuwasiliana na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa hatua zaidi, lakini pia hatua hiyo itausaidia Mfuko kuboresha huduma zake kwa wanachama na wananchi kwa ujumla,” alisema.