Meneja wa Twanga Pepeta aikimbia bendi, aenda Mashujaa

Baadhi ya wasanii wa Bendi ya Twanga Pepeta

Na Mwandishi Wetu

ALIYEKUWA Meneja Masoko wa Bendi maarufu na nguli ya African Stars Wana wa ‘Twanga na kupepeta’, Martine Sospeter jana ametangaza rasmi kujiunga na Bendi ya Mashujaa.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika mkutano na waandishi wa habari Sospeter, alisema maamuzi hayo yamekuja baada ya kuona hakutendewa haki na mwajili wake katika bendi hiyo.

Alisema majuzi usiku alishangazwa na kauli ya mkurugenzi wangu wa Asha Baraka katika vyombo mbalimbali vya habari kuwa amefukuza kazi kutokana kuhujumu bendi ikiwemo kushawishi wanamuziki kujiunga na bendi ya Mashujaa.

“Kwa kweli kauli ile ilinisikitisha sana kutokana na ukweli kwamba Asha nilimchukulia kama zaidi ya dada kwani nilifanya naye kazi kwa miaka 14 iweje hii leo aje anitolee maneno ya kunichafua katika vyombo vya habari wakati kuna ofisi”

Alisema yeye ajawahi kuhusika na mpango wowote wa wasanii wa Twanga kuhamia Mashujaa na wala hakuwa anafahamu mpango huo zaidi ya mwisho wa siku kusikia fununu za chini chini na mwishowe wasanii hao kutangazwa kuhamia Mashujaa. Mbali na mkataba baadhi ya makubaliano na uongozi wa mashujaa ni pamoja na kunipangia nyumba hali itakayonilazimu kuhama ile iliyokuwa chini ya Twanga.

“Leo (jana) napenda nitangaze rasmi kwamba nimeachana na African Stars na kujunga na Mashujaa Entertainment na tayari nimeshasaini mkataba wa kazi katika bendi hii ya Mashujaa ikiwa tayari nimeshahama katika nyumba ambayo nilipangishiwa na Twanga…ukweli sijapendezwa na kitendo cha dada yangu Asha,” alisema Sospeter.

Alisema ana amini atafanya vyema kazi yake hiyo mpya kama ilivyokuwa Twanga ambapo alidumu kwa muda mrefu na kuchangia kufika hadi hapo alipoachia, hivyo ameomba shirikiano kwa uongozi, wanamuziki, Wadau na hata na waandishi wa habari. Martine, ametambulishwa asubuhi hii katika mgahawa wa Business Park, Victoria, Dar es Salaam.

Pamoja na utambulisho huo, pia Martine amekanusha madai ya Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka kwamba ametoweka na fedha za bendi hiyo. Katika taarifa yake ya kumfukuza kazi Martine, Asha alidai Meneja huyo alichukua fedha kwa wateja kwa ajili kuwakodisha bendi- hivyo akamtaka azirejeshe. “Sijachukua fedha yoyote popote, sina deni, kama anadai nina deni, alete ushahidi,” alisema Martine.

Martine alisema kwamba kwa muda mrefu amekuwa akitakiwa na bendi ya Mashujaa kwa dau zuri, lakini amekuwa akikataa kutokana na jinsi anavyomheshimu Asha Baraka, lakini anasikitika amefukuzwa kwa kudhalilishwa.

“Amenikfukuza na kunitolea maneno ya kashfa mimi wakati nipo na bendi yake ziarani mikoani, imeniuma sana. Ila bado nitaendelea kumuheshimu Asha Baraka kama dada yangu na mtu ambaye amenifikisha hapa.” alisema Martine.

Sababu kubwa aliyoitaja Asha ya kumfukuza Martine ni kuwarubuni wanamuziki wa Twanga Pepeta kuhamia kwa wapinzani, Mashujaa. Miongoni mwa wanamuziki wa Twanga waliohamia Mashujaa ni mwimbaji hodari, Charles Baba.