Meneja Mkuu UDA amlipua Massaburi


Didas Massaburi

Na Mwandishi Wetu

SIKU moja baada ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam Dk. Didas Massaburi kutoa madai ya kusimamishwa kazi kwa Meneja Mkuu wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Victor Milanzi, meneja huyo ameibuka na kujibu kuwa madai hayo hayana ukweli bali yanalenga kumchafua na kummaliza.

Hali kadhalika Milanzi amedai kuwa Meya huyo pia amelenga kuficha ukweli na uchafu unafanyika dhidi ya shirika hilo akishirikiana na mmiliki wa Simon Group ambapo ndani kuna vigogo akiwemo waziri wa muda mrefu.

Meneja huyo pia amekanusha taarifa kuwa amesimamishwa kazi kwa kuwa hajapata barua rasmi ya kumsimamisha ila anachofahamu kuwa ofisi yake imevunjwa na Kampuni ya Simon Group ambao wameiba nyaraka muhimu zikiwemo hati miliki na kisha kuwaweka walinzi wao wa security.

Milanzi aliyatoa madai hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari akisisitiza kuwa yeye bado ni meneja pia hakuna ubadhirifu kwenye shirika hilo la usafirishaji. Wakati Milanzi akisisitiza hilo juzi Meya wa Jiji Dk. Massaburi aliwaambia waandishi wa habari kuwa Halmashauri ya Jiji imeridhia kusimamishwa kazi kwa meneja huyo kupisha kamati ya uchunguzi kumchunguza kwa tuhuma za ubadhirifu wa mamilioni fedha za UDA.

“ Nimeamua kuvunja ukimya wa muda mrefu baada ya Meya wa Jiji Didas Massaburi kuendelea kunichafua kwenye vyombo kadhaa vya habari kwa lengo la kuficha ukweli na uchafu anaoufanya akishirikiana na mmiliki wa Simon Group nimeona niweke wazi jambo hili, ” alisema Milanzi.

“ Naomba niweke mambo hadharani, kwanza nakanusha vikali taarifa za kwamba shirika la UDA kuna ubadhirifu wa sh. milioni 200 taarifa hizo Meya amezipata kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya Simon Group Robert Kisena ambao wametengeneza zengwe hilo ili kunichafua na kunimaliza, ”

Alibainisha kuwa wamilimi wa Kampuni ya Simon Group ni vigogo mbalimbali akiwemo waziri wa muda mrefu ambapo yeye (Milanzi) anavyo vielelezo ambavyo vinaonesha kuwa wanakusudia kulichukua UDA kwa nguvu ili kukidhi matakwa yao binafsi.

Alisema ikiwa ni kinyume cha taratibu Juni 10, mwaka huu Meya alibariki maamuzi ya bodi ya UDA kwa kufanya kikao na mmiliki wa kampuni hiyo akifahamu kuwa bodi ilikosea kwa kutowahusisha wanahisa wakubwa.

Alifafanua kuwa Dk. Masaburi alificha uchafu huo na kupitisha maamuzi yeye akijifanya Mwenyekiti, na Robert Kisena mmiliki wa kampuni hiyo kuwa katibu na kufanya maamuzi batili bila ya ridhaa ya Baraza la Madiwani pia bila ridhaa ya mwanahisa mkubwa ambaye ni hazina.

Alisema Meya hakuwa na Mamlaka ya kufanya hayo yote peke yake ambapo kabla alishauriwa na Mwenyekiti wa bodi kuwa UDA liko chini ya Consolidated Holding Corporation asifanye hayo anayoyafanya lakini hakutaka kumsikia.

Milanzi amesema analiomba Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam wasijitumbukize kupisha na kubariki hatua ambazo Meya Dk. Massaburi amezifanya kuwanyang’anya umma wa Watanzania mali zao ambazo wamekuwa wakizimiliki takribani miaka 38 na kuliacha Jiji bila usafiri wa uhakika.

Pili ameongeza kuwa anaiomba Serikali ambaye ndiye mmiliki wa UDA kupitia Msajili wa Hazina asikae kimya wakiangalia mali zikiporwa na watu ambao Mwalimu Nyerere alikuwa akiwaita manyang’au kwa visingizio mbalimbali.