Na Hassan Abbas, Addis Abbas
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe anatarajiwa kumsafishia njia Rais Jakaya Kikwete anayetarajiwa kuwasilisha na kuitetea Ripoti ya Hali ya Utawala Bora ya Tanzania mbele ya jopo la Marais wenzake wa Afrika wanaoshiriki Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM)
Wakati Rais Kikwete akitarajiwa kuitetea Ripoti ya Tanzania ya Hali ya Utawala Bora siku ya Jumamosi, Januari 26, 2013; Waziri Membe ambaye Wizara yake ndiyo inayoratibu shughuli za APRM nchini Tanzania anatarajiwa kuanza utetezi huo mbele ya Mawaziri na maofisa wengine waandamizi zaidi ya 100 kutoka nchi mbalimbali za Afrika katika mkutano wa utangulizi siku ya Ijumaa.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Rehema Twalib, Mkutano wa Ijumaa ni wa maandalizi kabla ya kikao cha Marais kinachofanyika Jumamosi. “Waziri Membe katika kikao hicho anatarajiwa kugusia matayarisho juu ya Rais kuwasilisha ripoti yake Jumamosi na ataeleza kwa kifupi juhudi za Serikali ya Tanzania katika kupambana na changamoto za utawala bora,” alisema.
Tayari ujumbe wa APRM Tanzania ukiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usimamizi, Prof. Hasa Mlawa, mjumbe wa Baraza hilo anayewakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano, John Magalle Shibuda na maofisa wengine waandamizi wa APRM wamekwishawasili jiji hapa kwa maandalizi ya mikutano hiyo.
Mpango wa APRM uliasisiwa miaka 10 iliyopita na Wakuu wa Nchi za Afrika kwa lengo la kuanzisha taasisi itakayokuwa na majukumu ya kufanya tathmini za mara kwa mara za hali ya utawala bora miongoni mwa nchi wanachama ili kuwashirikisha wananchi wao katika kujikosoa na kujisahihisha.
Taarifa iliyotolewa hivi karibu na APRM Makao Makuu, ilithibitisha kuwa Ripoti ya tathmini ya Tanzania iliyosheheni maoni ya wadau wa utawala bora Tanzania na majibu ya Serikali itawasilishwa katika kikao hicho.
“Ripoti ya Hali ya Utawala Bora ya Tanzania baada ya kukamilishwa inatarajiwa kujadiliwa mbele ya kikao cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika wanachama wa APRM kitakachofanyika Januari 26, 2013,” ilisema taarifa hiyo ya APRM makao makuu.
Akizungumza na watendaji wa APRM Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya mkutano huo, Rais Jakaya Kikwete alikaririwa jijini Dar es Salaam wiki iliyopita akisisitiza kuwa Serikali yake inaamini kuwa mchakato wa APRM hapa nchini ulifanyika kwa uwazi na kwamba yuko tayari kwenda kufanyiwa tathmini na wakuu wenzake wan chi za AU katika kikao hicho cha Jumamosi.