Membe Ampongeza Kikwete Kutekeleza APRM

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Na Hassan Abbas, Dodoma

RAIS Jakaya Kikwete amepongezwa kwa nia yake ya dhati katika kutekeleza Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) ambapo Januari mwaka huu aliiwasilisha Ripoti ya Tanzania mbele ya Wakuu wa Nchi za Afrika mjini Addis Ababa.

Pongezi hiyo zilizoelekezwa pia kwa mwakilkishi wa Bunge katika APRM, John Shibuda zilitolewa Jumamosi Bungeni mjini hapa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Waziri Membe alikuwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge kuhusu bajeti ya wizara yake na taasisi zilizoko chini ya wizara hiyo ambapo APRM ni mojawapo. Alisema kitendo cha Rais kuwasilisha Ripoti hiyo Addis Ababa, kuitetea na kukubalika mbele ya viongozi wa Afrika ni heshima kubwa kwa nchi yetu.

Alimpongeza mbunge Shibuda pia kwa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa APRM hapa nchini. “Kazi tuliyo nayo mbele yetu kwa sasa ni kutekeleza Mpangokazi wa kitaifa ambao sasa ni jukumu letu kama nchi,” alisema Waziri Membe.

Katika majibu yake kuhusu hoja za wabunge, Waziri Membe pia alisisitiza kuwa katika kuimarisha shughuli za APRM Tanzania, Serikali pia itaipatia taasisi hiyo kasima yake ili iweze kudhibiti matumizi yake ya fedha kwa urahisi.

Hoja ya kuipatia APRM kasima yake ilitolewa na Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo ambaye alisema kupatikana kwa kasima ndogo kutasaidia APRM kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi zaidi.

Awali Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa wizara hiyo, Ezekia Wenje aliishauri Serikali kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa kwenye Ripoti ya APRM mara baada ya Rais kuwa ameiwasilisha Ripoti hiyo na kuitetea mbele ya wakuu wenzake wan chi za APRM.

Akiwasilisha makadirio na utekelezaji wa shughuli za wizara yake juzi, kabla ya Bunge kuahirishwa mara kadhaa, Waziri Membe katika hotuba yake kwa Bunge, alisema Serikali itahakikisha Ripoti ya APRM inatekelezwa.

“Nchi yetu ilihimizwa kuzifanyiakazi changamoto za migogoro ya wakulima na wafu-gaji, imani za kishirikina, kuhakikisha manufaa ya kukua kwa uchumi yanawafikia wananchi na kutoa elimu kwa umma kuhusu Mipango na Sera za Serikali,” alisema.

Waziri Membe alizitaja kazi zijazo za Mchakato wa APRM hapa nchini kuwa ni Serikali kuanza kazi ya kutekeleza maoni na mapendekezo ya  Ripoti ya APRM kwa kuingiza mapendekezo hayo katika Mipango ya Serikali.

APRM ni Mpango wa uliobuniwa na viongozi wa Nchi za Afrika miaka 10 iliyopita na taasisi hiyo kuanzishwa katika nchi mbalimbali za Afrika. Tanzania iliyojiunga na APRM mwaka 2006 kwa sasa ni miongoni mwa nchi 33 wanachma wa APRM kati ya 54 za Umoja wa Afrika (AU).

Tamko la Waziri Membe Bungeni pia ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kwa kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa APRM kutoka AU waliokuja kuhakiki zoezi la Tanzania kujitathmini ambapo aliwaahidi Serikali yake kufanyiakazi mapendekezo yatakayotolewa.