Mechi za Raundi ya 21 na 22 Kusimama Kupisha Viporo vya Polisi

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
MECHI za raundi ya 21 na 22 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa makundi yote zitasimamishwa ili kupisha Polisi Mara imalize mechi zake za viporo, na timu zote zicheze mechi zao za raundi zilizobaki kwa pamoja. Polisi Mara ilifungiwa kutumia Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma kutokana na vurugu zilizojitokeza kwenye mechi zake, hivyo kusababisha kuwepo kwa mechi hizo za viporo dhidi ya JKT Kanembwa na Polisi Tabora.

Tayari Polisi Mara tumeiruhusu itumie tena Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kwa mechi zake za nyumbani baada ya kuipa onyo kali kutokana na vurugu hizo. Lakini pia mechi zake kwenye uwanja huo zitachezwa chini ya uangalizi.

Uamuzi wa kupisha Polisi Mara imalize mechi zake za viporo una lengo la kuhakikisha mechi zote za raundi tatu za mwisho zinachezwa pamoja ili kuepuka uwezekano wa kupanga matokeo. Pia klabu za FDL zenyewe ziliwasilisha ombi la kutaka mechi hizo za mwisho zichezwe kwa wakati mmoja.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) wakati wowote kuanzia kesho (Januari 27 mwaka huu) itatoa ratiba ya mechi za viporo za Polisi Mara, pamoja na tarehe mpya za mechi za raundi ya 20, 21 na 22.

ROBO FAINALI KOMBE LA TAIFA WANAWAKE KUANZA KESHO
Hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Taifa kwa Wanawake inachezwa kesho (Januari 26 mwaka huu) na Januari 27 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam kwa mechi mbili kila siku.

Mechi ya kwanza ya robo fainali ya michuano hiyo itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Televisheni itaanza saa 9 alasiri kwa kuzikutanisha Mwanza na Kigoma. Robo fainali ya pili ambayo ni kati ya Tanga na Pwani itaanza saa 11 kamili jioni.

Ilala na Iringa watacheza robo fainali ya tatu Januari 27 mwaka huu kuanzia saa 9 kamili alasiri, na kufuatiwa na robo fainali ya mwisho saa 11 kamili jioni itakayozikutanisha Temeke na Mbeya.

Nusu fainali za michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Proin zitachezwa Januari 29 mwaka huu wakati Fainali itachezwa Februari Mosi mwaka huu kuanzia saa 10.15 jioni ambapo itatanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu (play off). Timu zote zilizoingia hatua hiyo ya nane bora ya michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini zimefikia hosteli ya Msimbazi.

Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litakuwa na mkutano na waandishi wa habari. Mkutano huo utafanyika kesho (Januari 26 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)