Mechi ya Yanga na African Lyon yaingiza mil 26.2

Mechi ya Yanga na African Lyon

Na Mwandishi Wetu

MECHI namba 126 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na African Lyon iliyochezwa Machi 14 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 26,216,000. Jumla ya watazamaji 7,636 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 3,000 viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B wakati kwa VIP A ilikuwa sh. 15,000.

Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 3,999,050.85 kila timu ilipata sh. 3,752,924.75, uwanja sh. 1,250,974.92.

Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 500,389.97, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 1,250,974.92, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 625,487.46, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 125,097.49 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni sh. 1,250,974.92.

Gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000. mwamuzi wa akiba sh. 30,000, posho ya kujikimu kwa waamuzi sh. 80,000, tiketi sh. 3,000,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.

Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 534,520 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 458,160.

Wakati huo huo; mkutano kati ya Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na waandishi wa habari uliokuwa umepangwa kufanyika leo (Machi 15 mwaka huu) saa 6 kamili mchana kwenye ofisi za Shirikisho umeahirishwa mpaka utakapotangazwa tena. Sababu ya kuahirisha mkutano huo imetokana na kuwepo kwa mkutano mwingine wa waandishi wa habari za michezo ulioitishwa katika muda huo huo na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.