CHAMA cha Mpira wa Miguu Sudan (SFA) kimefuta mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na timu ya Taifa ya nchi hiyo ‘Nile Crododile’ iliyokuwa ichezwe Agosti 10 mwaka huu.
Uamuzi huo umetokana na wakala wa mechi hiyo Hadi Sharkawy kushindwa kupata kwa wakati tiketi ya kuisafirsha Taifa Stars kwenda Khartoum. Pia kutokana na mechi hiyo kufutwa, kambi ya Stars iliyokuwa hapa Dar es Salaam nayo imevunjwa leo.
Wakati huo huo Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji iliyokutana Agosti 7 mwaka huu kupitia masuala mbalimbali imeiagiza klabu ya African Lyon iwe imewalipa wachezaji wake wawili kufikia Agosti 17 mwaka kwa kuvunja mikataba yao na klabu hiyo. Wachezaji ambao kila mmoja anadai sh. milioni 4.3 ni Godfrey Komba na Abdul Masenga.
Awali kamati hiyo katika kikao chake cha Januari 7 mwaka huu iliagiza klabu hiyo kutosajili mchezaji mpya msimu wa 2011/2012 hadi itakapokuwa imemaliza suala la wachezaji hao. Lyon imeomba kusajili wachezaji wapya wanane kati ya 23 inayotaka kuwatumia kwa msimu mpya.
Kwa kuzuiwa kusajili wachezaji wapya iwapo haitakuwa imemalizana na Komba na Masenga kufikia Agosti 17, Lyon itakuwa imebaki na wachezaji 15 hivyo kikanuni kutokuwa na sifa ya kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom. Kanuni inaagiza timu inayoshiriki ligi hiyo kuwa na wachezaji wasiopungua 18 na kuzidi 30.