Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua waamuzi kutoka Rwanda kuchezesha mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania Kombe la Shirikisho kati ya Simba na ES Setif itakayochezwa Machi 25 mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, mwamuzi wa kati ni Hudu Munyemana wakati wasaidizi wake ni Felicien Kabanda, Theogene Ndagijimana na Edouard Bahizi. Kamishna wa mechi hiyo ni Felix Tangawarima kutoka Zimbabwe.
Wambura amesema mechi hiyo namba 45 itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni. Mechi ya marudiano ambayo ni namba 46 itachezwa Aprili 6 mwaka huu nchini Algeria.
Iwapo Simba itafanikiwa kusonga mbele itacheza mechi ya kwanza nyumbani Aprili 29 mwaka huu na mshindi kati ya El Ahly Shandy ya Sudan na Ferroviario de Maputo ya Msumbiji ambapo ya marudiano itachezwa kati ya Mei 11, 12 na 13 mwaka huu.