Mechi ya Simba, Mtibwa zaingiza mil. 74

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Mtibwa Sugar iliyochezwa Septemba 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 74,345,000.

Akizungumza na wanahabari leo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura amesema watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 13,285 ambapo kiingilio kilikuwa sh. 5,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 7,000 rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B na sh. 20,000 kwa VIP A.

Eneo lililoingiza watazamaji wengi ni kwenye viti vya bluu na kijani ambapo waliingia 11,798 wakati lililoingiza watazamaji wachache ni la VIP A ambapo waliingia 58. Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo ambazo ni sh. 11,637,000 na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 11,340,762.70 kila timu ilipata sh. 15,410,171.19.

Mgawo mwingine ulikwenda kwa gharama za mchezo (sh. 5,136,723.73), uwanja (sh. 5,136,723.73), TFF (sh. 5,136,723.73), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 2,568,361.86), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh. 2,054,689.49) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 513,672.37).