Mechi ya Bongo Movie, Twiga Stars sasa Mei 4, 2012

Baadhi ya wachezaji wa timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars)

MECHI maalumu ya hisani kwa ajili ya kuchangia timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars), kati ya timu hiyo na wasanii wa filamu maarufu kama Bongo Movie itachezwa Mei 4 mwaka huu.

Kwa mujibu wa kampuni ya Edge Entertainment iliyoandaa mechi hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni kwa kiingilio cha sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.

Twiga Stars kwa sasa hivi haina mdhamini na iko kambini katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Ruvu mkoani Pwani inashiriki michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) ambapo Mei 26 mwaka huu itacheza na Ethiopia jijini Addis Ababa. Fainali za AWC zitafanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.

Wachezaji wawili Watanzania wameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya kucheza mpira wa miguu katika nchini za Denmark na Jamhuri ya Czech.

Wakati huo huo, chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU) kimemuombea hati hiyo William Benard Okum kama mchezaji wa ridhaa ili ajiunge na timu ya Brabrand IF. Klabu ya zamani ya Okum ni Viko Pham FC ya Zanzibar.

Naye Samwel Jonathan Mbezi ameombewa hati hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu cha Jamhuri ya Czech (FACR) ili aweze kuchezea timu ya Sokol Dolany akiwa mchezaji wa ridhaa. Katika maombi hayo, FACR imeonesha kuwa Mbezi kwa sasa hana timu anayochezea hapa nchini.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanya mawasiliano na pande husika kabla ya kutoa hati hizo kwa wachezaji hao kama walivyoomba DBU na FACR.