MCT Yaliamuru Dira ya Mtanzania Kumlipa Lowassa kwa Kumkashfu

Gazeti la Dira ya Mtanzania

Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) imeliamuru Gazeti la Dira ya Mtanzania kumlipa fidia aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa baada ya kuchapisha taarifa za kumkashfu kiongozi huyo bila kumpa nafasi ya kujibu. Uamuzi huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya MCT, Jaji Thomas Mihayo baada ya kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Jijini Dare es Salaam Septemba 20, 2012.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, alisema madai yaliyochapishwa na gazeti hilo ya kumuhusisha Mkuu wa Nchi (Rais Kikwete) na Lowassa yanaudhi, yanadhalilisha na yanaleta dharau. Jaji Mihayo alisema Novemba 11, 2011 mawakili wa kampuni ya Imma Advocates, wawakilishi wa Lowassa waliwasilisha malalamiko ya mteja wao kwa kamati hiyo.

Waziri mkuu huyo wa zamani alikuwa analalamikia zaidi ya habari sita ambazo zilimkashifu zilizochapishwa na gazeti hilo; habari ya kwanza ilichapishwa katika Dira ya Mtanzania toleo na 120 la Oktoba 6 – 9, 2011 iliyokuwa na kichwa cha habari Lowassa, Chenge tena” ikifuatiwa na habari mbili katika toleo na 123 la Oktoba 17-19, 2011 kwenye ukurasa wa kwanza zikiwa na vichwa vya habari Nape atonesha kidonda – akumbusha Mwalimu alivyomkataa Kapteni Lowassa na Kapteni Lowassa atajwa kwenye vurugu za CCM Arusha.

Alisema katika toleo la 125 la Oktoba 24-26, 2011 ukurasa wa kwanza gazeti hilo lilichapisha habari Kapteni Lowasa, Kikwete basi. Katika toleo la Oktoba 31- Novemba 1, 2011 ukurasa wa kwanza gazeti hilo lilichapisha habari yenye kichwa Kapteni Lowassa anaandaa mashitaka wakati katika toleo 128 la Novemba3-6, 2011 pia kwenye ukurasa wa kwanza, lilichapisha habari yenye kichwa Askofu Mokiwa amkana Kapteni Edward Lowassa. Gazeti hilo pia lilichapisha habari kwamba CCM yapambana na Kapteni Lowassa.

Akiwasilisha shauri lake mbele ya Kamati hiyo ya maadili yenye wajumbe watatu, Lowassa alisema kuwa maombi yake kadhaa kwa gazeti hiloya kutaka kuweka sawa habari hizo na kuzikanusha hayakushughulikiwa. Kuhusu madai kuwa Lowassa anakosana na Rais Kikwete, Jaji alisema kitendo hicho kilichoelezwa na gazeti hilo ni cha hatari kwani ni uhaini kutofautiana hadharani na mkuu wa nchi. “Kama rais angekuwa mtu mwingine anayefuata habari za magazeti unatiwa ndani”, alisema.

Jaji Mihayo alikubaliana na suala hilo hivyo kulitaka Dira ya Mtanzania kumuomba radhi Lowasa na kumlipa fidia zote alizoingia katika shauri hilo. Katika kikao hicho kamati hiyo pia ilitoa uamuzi kwa malalamiko ya kampuni ya Human Capital Investment Group Limited dhidi ya gazeti la Rai toleo namba 966 la April 5, 2012.

Katika shauri lingine gazeti la Rai limelalamikiwa kwa kuchapisha katika toleo lake la Aprili 25, 2012 kuwa TGNP yatapeliwa 270 mil/- Bagamoyo. Yanunua kiwanja kilichopo eneo la EPZ. Iliuziwa na kampuni ya Human Capital Investiment.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Zuhura Muro ambaye aliiwasilisha mbele ya kamati hiyo alisema kuwa taarifa ya gazeti hilo imeichafua kampuni hiyo na vile vile kumharibia sifa yeye na hata familia yake. Mhariri Mtendaji wa New Habari inayochapisha gazeti hilo la Rai Prince Bagenda alikiri kuwa gazeti hilo lilikosea na akaahidi kuchapisha taarifa ya kuomba radhi.Kamati hiyo ya MCT iliamuru kampuni hiyo kuomba radhi kwenye ukurasa wake wa kwanza.