Mchezo wa Ngumi Unavyopoteza Uasili Wake (Sehemu ya 12)

Onesmo Ngowi

Na Onesmo Ngowi

MASUMBWI au kwa jina lingine ndondi ni mchezo unapoendwa sana na watu wengi. Aidha mchezo huu ni kati ya michezo inayoogopwa sana duniani. Mchezo wa ngumi uko hatarini kupoteza maana yake ya asili yaani kucheza kama burudani, kuwakilisha nchi na kujenga ushupavu wa mchezaji. Mamilioni ya watu wanaojazana kuutazama wasingependa kabisa kujiingiza kuucheza mchezo wa ngumi. Sasa endelea….!

Mabadiliko makubwa katika mchezo wa ngumi yalianza kutokea katikati ya miaka ya 50 kuelekea kwenye miaka ya 60. Mchezo wa ngumi ambao ulikuja kutawaliwa sana na makundi ya wahalifu (Mafia) ulianza kupata msukumo na kasi baada ya makampuni mengi ya biashara kuanza kujiingiza kuidhamini.

Miaka ya nyuma ngumi haswa katika nchi za Amerika ya Kaskazini na Ulaya zilichezwa kwenye kumbi au viwanja vya wazi na pato pekee lililopatikana lilikuwa ni viingilio vya milangoni na kamari ambazo zilikuwa zinatolewa na watanzamaji wakitabiri bondia atakayeshinda. Makundi mengi ya wahalifu (Mafia) yalitumia njia ya kamari kujipatia fedha nyingi sana kwenye mapambano ya ngumi.

Mara nyingi makundi haya ya uhalifu yalipanga matokeo ya mapambano ili yafaidike na fedha za kamari. Hii ilitegemea na bondia yupi watu wengi walimtabiria kushinda kwa hiyo walihonga bondia shupavu apoteze ili waweze kuchukua fedha nyingi. Kamari hizi (betting) bado zinatumika katika nchi nyingi za Ulaya na Amerika ya Kaskazini mpaka leo lakini kwa njia ya kawaida inayokubalika na mifumo ya pesa ya nchi zenyewe.

Mwishoni mwa miaka ya 50 na haswa wakati mabondia kama kina Sonny Liston, Rocky Marciano, Joe Loius na Jack Dempsey wakiwa kwenye chati ngumi zilianza kupata ushirikiano wa makampuni ya biashara yaliyodhamini mapambano mbalimbali.

Wamarekani wengi weupe wakati bondia Rock Marciano, mwamerika mweupe akiwa kwenye chati alionekana kama ni tegemeo kubwa kwao kwani kwa kipindi kirefu watu weusi ndio waliotawala sana mchezo wa ngumi haswa kwenye uzito wa juu (heavyweight). Rocky Marciano ambaye baadaye alikuja kufa kwenye ajali ya ndege alikuwa na ushindi wa mapambano 49 bila kupoteza hata pambano moja.

Katikati ya miaka ya 60 mchezo wa ngumi za kulipwa ulianza kupata msisimko wa kipekee baada ya bondia Cassius Clay ambaye alikuja kubadili jina na kuitwa Muhammad Ali kujiunga nayo. Makampuni mengi yanayotengeneza bidhaa mbalimbali yalijiingizia kwenye udhamini wa ngumi. Hali kadhalika mapromota wakubwa nao walianza kujitokeza kuendesha michezo wa ngumi kibiashara.

Ni katikati ya miaka ya 60 kuelekea kwenye miaka ya 70 wakati pambano moja la ngumi bondia aliweza kujizolea mamilioni ya dola za Kimarekani. Pengine ubunifu na mbinu kubwa za biashara za mapromota kama Don King, Bob Arum, Mickey Duff, Frank Waren na wengine wengi yaliwezesha kufikia mafanikio haya.

Mapromota mbalimbali waliweza kujitokeza kuwanufaisha mabondia wengi. Ijulikane kwamba mabondia wengi maarufu na waliopata fedha nyingi walikuwa wa uzito wa juu (heavyweight). Baadhi yao wakiwa: Muhammad Ali, Joe Frasier, Floyd Perterson, Achie Moore, Ken Norton, Joe Burger, George Foreman, Jacky Quary, Leon and Michael Spinks na wengine wengi.

Katikati ya miaka ya 70 na 80 mabondia wengi wa uzito wa kati nao waliweza kujizolea fedha nyingi katika mchezo wa ngumi. Mabondia hawa ni pamoja na Marvin Hugler, Sugar Ray Leornard, Tommy Hearns, Roberto Duran, Alfred Benitez n.k. Miaka ya karibuni na ya sasa mabondia wa kati waliolipwa/wanaolipwa fedha nyingi wanaongozwa na kina Manny Pacquiao Floyd Mayweather, Bernard Hopkin, Oscar De Laroya, Felix Trinidad n.k.

Pengine jambo moja ambalo lazima kueleweka ni kwamba mafanikio yote haya yalitokea kwa sababu mabondia wahusika walikuwa na viwango vizuri vya ngumi. Walikuwa pia na safu nzuri ya uongozi kuanzia meneja, kocha, daktari na wengine. Wengi wa mabondia hao waliotajwa hapo juu walitokea kwenye mashindano makubwa ya kimataifa pamoja na Olimpiki. Wengi wao walijiunga na ngumi za kulipwa baada ya kushinda medali za dhahabu za Olimpiki.

Mfumo mzuri wa biashara uliwawezesha kuwanufaisha sana mabondia hao na hivyo kuweka msingi mzuri wa promosheni kubwa za ngumi duniani. Kilichotokea baada ya miaka ya 80 ni ushiriki mkubwa wa makampuni ya biashara na mitandao mikubwa ya television duniani kujiingiza kwenye promosheni na udhamini wa ngumi.

Tanzania inaweza kufikia viwango vikubwa sana vya ngumi kama television zetu pamoja na makampuni ya biashara yataanza kujiingiza kudhamini mchezo wa ngumi na huu ukawa mwanzo wa kuinua mchezo huu. Mawazo kwamba ugomvi au migogoro katika mchezo wa ngumi yanadidimiza ngumi sio kweli.

Kwa kuanzia tu ni kwamba chama cha ngumi sio promota au meneja wa bondia. Uhusiano wa meneja au promota wa ngumi na chama ni kwa ajili ya kupata leseni na kibali cha mchezo wa ngumi. Chama cha Ngumi hakina wajibu wa kumtafutia bondia pambano. Promota wa ngumi hawezi kuwasiliana na chama cha ngumi kwa ajili ya kushirikiana nacho kuandaa pambano. Chama cha ngumi hakimiliki bondia.

Bondia mwenyewe ni mfanyabiashara na uhusiano wake tu na Chama ni kupata leseni ya kucheza pamoja na kibali. Uhusiano wao ni kama mtoza kodi na mlipa kodi. Lakini zaidi ya kutoza kodi Chama husimamia kanuni, taratibu na sheria za mchezo wa ngumi. Kinawapatia mabondia leseni za kucheza, mameneja, promota, refarii, majaji na wahusika wote wa ngumi leseni na vibali vya kuendeshea shughuli zake.

Bondia akipanda ulingoni anachukua kundi zima kuanzia promota, meneja, kocha, refarii, jaji, cutman, daktari, timekeeper, mpiga kengele, ring announce n.k. Bila bondia watu wote waliotajwa hapo juu hawana kazi. Lakini bondia anaweza kucheza bila baadhi ya waliotajwa hapo juu.

Katika utaratibu mzuri na wenye manufaa kwa bondia ni muhimu awe na watu wafuatao: Meneja, kocha, daktari na wakili. Hawa ni watu muhimu sana kwa maendeleo ya bondia. Meneja ndiye anayehakikisha kwamba bondia anapata mapambano mara kwa mara na analipwa fedha nzuri. Kocha anahakikisha kwamba bondia yuko kwenye hali nzuri ya kushindana kwa kumpatia programu nzuri ya mazoezi. Daktari atahakikisha kwamba bondia yuko kwenye hali nzuri kiafya kucheza. Wakili atahakikisha kwamba atamshauri vizuri bondia kwenye mikataba na ni kampuni ipi nzuri ya bima itakayompa kinga.

Mabondia wa Tanzania wanatakiwa wacheze ngumi kwenye mfumo huu wa kisasa kwa manufaa yao. Lakini ni muhimu jamii ikaelimishwa kuhusu umuhimu na manufaa ya kujiingiza katika nafasi mbalimbali za kuendeleza mchezo wa ngumi ili kusaidia mchezo wenyewe na kujiendeleza kibiashara. Hii itakuwa na manufaa kwa wote. Ni dhana potofu kufikiria kuwa mchezo wa ngumi ni wa watu ambao hawajawahi kwenda shule.

Katika nchi za wenzetu watu wengi walio na elimu ya juu hujishughulisha na ngumi. Watu hawa ni pamoja na mawakili, madaktari, mainjinia, walimu, mapolisi n.k

Kama nilivyosema hapo mwanzo kuwa viwango vya mabondia katika uchezaji wao ni muhimu sana. Viwango hivi (standards) ndivyo vinavyowahakikishia kupata mapambano yenye fedha nyingi ndani na nje ya nchi.

Bondia anatakiwa ajitume ili ajiweke kwenye hali nzuri ya mchezo wake wa ngumi na hatimaye kujihakikishia malipo mazuri pamoja na nafasi nzuri kwenye viwango vya kimataifa. Bondia anatakiwa ajue kuwa jamii inamwangalia kwa jicho la kumtukuza kwa kuwa kwa wengi yeye ni shujaa na mfano wa kuigwa. Hivyo mbali na kiwango kizuri cha ngumi anatakiwa pia aishi maisha yanayoweza kuigwa na wengi katika jamii hususan vijana.

Kwa bahati mbaya mabondia wengi duniani pamoja na Tanzania ni watu waliotoka kwenye familia zenye vipato vya chini. Wengi wao hawana elimu ya kutosha na hivyo kuwanyima uwezo mkubwa wa kujipangilia maisha yao nje ya ulingo. Uwezo duni wa elimu unawafanya wasiweze kutumia vyema fedha wanazopata kwenye mapambano ya ngumi.

Udhaifu huu unafanya wengi wa mabondia ama kudanganywa fedha nyingi na watu wanaowasimamia (mameneja na mapromota) au wao wenyewe kuchezea fedha hizo kwa kuzitumia kwenye anasa na kujionyesha.

Mfano mmoja mzuri ni maisha ya nje ya ulingo ya bondia aliyekuwa maarufu duniani Mike Tyson. Kama inalivyokwisha andikwa na vyombo vingi vya habari maisha ya bondia huyu yalikuwa ni kitendawili. Pamoja na fedha nyingi alizowahi kupata kwenye mapambano mbalibali ya ngumi katika uhai wake inasemekana kwamba bondia huyu kwa sasa amefilisika. Hali yake iko mikononi mwa wasamaria mbalimbali.

Kila pambano alilocheza kwa miaka yake ya mwisho wa ngumi na fedha alizokuwa anazipata alikuwa analipia madeni aliyokuwa anadaiwa. Madeni hayo yanaanzia kwenye kodi ya serikali ya nchi yake, mikopo ya vitu mbalimbali kama nyumba, magari, vito vya thamani, nguo n.k. Madeni mengine ni pamoja na fedha za kulipia familia ya mke wake wa zaman ambaye waliachana na ana watoto wawili naye. Fedha hizo zinatakiwa zipatikane ili kuweza kuitunza familia hii.

Inavyokadiriwa na wengi kwamba Mike Tyson alishawahi kutengeneza kiasi kilichozidi dola milioni 800 za kimarekani. Kiasi hiki hapa kwetu Tanzania ni zaidi ya makusanyo ya kodi ya serikali kwa mwezi nchi nzima. Ni fedha ambazo nchi nyingi duniani hazina kwenye benki zao kuu. Ukosefu wa elimu ulioendekeza matumizi mabaya yaliyokithiri ndiyo yaliyomfanya bondia Mike Tyson kupoteza fedha zake nyingi.

Inasemekana kwamba matumizi yake ya siku wakati alipokuwa aking’ara yalikuwa zaidi ya dola laki moja na nusu za kimarekani sawa na shilingi milioni mia mbili na ushee za kitanzania. Hata kama una mashine za kutengeneza fedha matumizi kama haya kwa hakika yatakupeleka pabaya.

Hapa kwetu Tanzania hali ya mabondia wetu haina tofauti na hii ya bondia Mike Tyson. Mabondia wetu wengi ni wale walioweza tu kupata elimu ya msingi na baadhi yao hata hawakufika darasa la saba. Mfumo mzuri wa michezo hapo nyuma uliwahakikishia maisha mazuri kwa kuchukuliwa na mashirika mbalimbali yaliyohitaji vipaji vyao. Mfumo huu ulisimama baada ya mashirika mengi kubadili mifumo ya kujiendesha na mengine kufa kabisa. Wengi wao walikosa kazi na kujikuta wakijitegemea wenyewe kulisha familia zao.

Vijana wengi wenye vipaji vya michezo kwa sasa hawapati tena nafasi ya kuajiriwa na mashirika mengi isipokuwa idara chache tu za serikali kama Polisi, Magereza, Uhamiaji n.k. Mabadiliko makubwa ya mifumo ya uendeshaji wa mashirika ya umma yamechangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha maendeleo ya michezo hususani mchezo wa ngumi.

Lakini kwa wachache waliocheza ngumi za ridhaa na baadaye kujiunga na ngumi za kulipwa maisha yao hayana tofauti kubwa. Wengi wanaopata nafasi ya kucheza mapambano ya kimataifa huenda tu kwa ajili ya kupata fedha za kujikimu na sio kushindana. Wengi wao hawana hata uwezo wa kujiandaa kwa mapambano haya.

Inatokea mara nyingi mabondia kupata nafasi za kucheza nje ya Tanzania na kupigwa kirahisi sana. Wengi wao hata hawapigwi ila wanasalimu amri kwa kujirusha chini au kukataa kuendelea. Kwa kuwa mchezo wa ngumi za kulipwa unachezwa kwa mikataba ambayo haisemi kama fedha anazolipwa bondia zinategemea anaposhindwa au kushinda huwa wanalipwa fedha zao zote pambano linapomalizika.

Lakini kidogo wanacholipwa huanzia dola elfu moja hadi elfu hamsini (shilingi milioni moja hadi milioni hamsini) wanaporudi nyumbani na kitita cha fedha zao wanahamia kwenye majumba ya starehe na wengine huenda kwenye fukwe za kitalii kisiwani Zanzibar ili waende na wakati kwenye ulimwengu wa anasa. Wengi wao wanaporudi nchini hujificha hadi mikoba yao inapokauka kabisa ndipo hujitokeza na kulia njaa.

Wapo mabondia waliokwisha rudi nyumbani na kitita cha uhakika na kutokomea Zanzibar ambako walizifanyia fujo fedha zao kama vile ulimwebu unaisha. Baada ya wiki chache walirudi Dar Es Salaam na kupiga hodi kwenye ofisi za TPBC kuomba nauli ya daladala. Iaendelea….!

Mwandishi wa makala haya ni; Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC), Shirkisho la Ngumi za Kulipwa Afrika Mashariki na Kati (ECAPBF), Shirikisho la Ngumi la Kimataifa bara la Afrika, Masharilki ya Kati, Ghuba ya Uarabu na Uajemi (IBF/AFRICA) na Mkurugenzi wa Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) E-mail: ibfafrica@yahoo.com.