Nchi ya Uingereza iko mbioni kumzuia nyota wa Arsenal Alex Iwobi asijiunge na timu ya Super Eagles ya Nigeria.
Hii ni kutokana na kauli ya chipukizi huyo ya kuasi timu ya taifa ya Uingereza na badala yake kujiunga na vigogo wa soka ya Afrika Super Eagles ya Nigeria.
Iwobi ameshajumuishwa katika kikosi cha Nigeria kinachoratibiwa kuchuana dhidi ya Misri siku ya Ijumaa 26 -29 Machi katika mechi ya kufuzu kwa kombe la mataifa ya Afrika.
Uingereza imeanza harakati za kumshawishi asijiunge na Nigeria kwani hilo litawanyima fursa ya kumshirikisha katika timu ya taifa ya England.
Iwobi mwenye umri wa miaka 19 aliichezea England katika mashindano ya dunia ya vijana wasiozidi umri wa miaka 16,17 na hata 18 kabla ya kuamua kuwa angependa kuiwakilisha taifa alikozaliwa yaani Nigeria kuambatana na kanuni za FIFA.
Jarida la Daily Mirror linaripoti kuwa harakati za kimya kimya zinafanywa ilikumshawishi Iwobi abadilishe kauli yake kabla ya Ijumaa, kwani akishaichezea Super Eagles itakuwa vigumu mno kuichezea England katika mechi za kimataifa.