Mchango wa Kabwe Zitto Kwenye Bajeti ya Serikali Mwaka 2014/15

Mbunge wa Kigoma Kaskazini(Chadema), Kabwe Zuberi Zitto.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini(Chadema), Kabwe Zuberi Zitto.


MCHANGO WA MAANDISHI WA NDG. KABWE ZUBERI ZITTO, MB KUHUSU BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA WA FEDHA 2014/2015

MHESHIMIWA Spika, Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nguvu za kuweza kuandika mchango wangu huu mdogo kwenye mjadala wa Bajeti ya Serikali mwaka 2014/15. Kama wengi mnavyofahamu mnamo tarehe 1 Juni mwaka 2014 nilimpoteza mama yangu mzazi na kumsitiri siku iliyofuata tarehe 2 Juni, 2014. Huu ni msiba mkubwa sana kwangu na ndugu zangu wote kwani mama yetu Bi. Shida Salum alikuwa nguzo katika familia. Nafahamu kuwa jamaa na marafiki wa mama pia wamepoteza mtu wao muhimu sana. Napenda kuwashukuru nyote kabisa kwa salamu zenu za pole kwetu. Sina namna ya kuelezea shukrani zangu kwenu kwani Bi Shida kwangu alikuwa zaidi ya mama mzazi, alikuwa rafiki, dada na nguzo. Ninamshukuru Allah kwa kuniwezesha kumwuguza na kumsitiri mama yangu. Hakuna amali kubwa ambayo Mungu amenipa zaidi ya hiyo. Nawashukuru tena nyote kabisa wabunge wenzangu kwa kushirikiana nami kwa namna zozote zile kumwuguza na kumsitiri mama yangu. Mungu atawalipa malipo yanayowastahili kwa amali na vitendo vyenu. Sisi kama familia tutaendelea kumwombea dua mama yetu na kumtolea sadaka ili ahifadhiwe mahala pema.

Mheshimiwa Spika, ningependa niwe nanyi katika mjadala huu muhimu wa kila mwaka wa Taifa letu. Hata hivyo bado Mungu hajaniwezesha nguvu za kusimama na kuzungumza. Pindi nitakapowezeshwa nguvu hizo nitakuwa nanyi kwa kipindi hicho nitakachojaaliwa ili kushiriki katika kazi za kuendeleza Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kumpongeza Waziri wa Fedha ndugu Saada Salum kwa kuwasilisha Bajeti yake ya kwanza kabisa kama Waziri wa Fedha wa pili Mwanamke wa nchi yetu. Nampongeza kwa kuchukua hatua kadhaa za kuboresha usimamizi wa fedha za umma na hasa matamko aliyotangaza ya kupambana na misamaha ya kodi ambayo imeongezeka mpaka kufikia asiliamia 3.5 ya Pato la Taifa na asilimia 10 ya Bajeti ya Serikali.  Misamaha ya Kodi mwaka 2012/13 ilifikia tshs 1.5 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 15 ya makusanyo yote ya ndani na ni sawa na takribani fedha zote za kodi ambazo Serikali ilikusanya kama kodi ya mishahara ya Wafanyakazi (PAYE). Hata hivyo, matamko ya Serikali yana mapungufu makubwa sana na ni matamko yale yale yanayorudiwa kila mwaka bila utekelezaji. Kuweka wazi misamaha ya kodi na watu au asasi zilizofaidika na misamaha hiyo ni hatua nzuri lakini haitoshi kama hatua hiyo haitaendana na kufanya ukaguzi wa misamaha hiyo. Kamati ya Bunge ya PAC ilitoa agizo mwaka 2013 la kutaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kukagua misamaha ya kodi kama matumizi mengine yeyote ya Serikali. Ieleweke kwamba misamaha ya kodi ni ruzuku (subsidy), ni fedha ya Serikali ambayo iwapo ingekusanywa ingekaguliwa kwa mujibu wa sheria. Matamko ya Serikali ya kuweka wazi misamaha lazima yaendane na kuifanyia ukaguzi (auditing) na kuweka wazi matokeo ya ukaguzi huo. Vilevile ni lazima sasa katika Sheria ya Fedha ya mwaka 2014/15 kuweka kipengele cha kuzuia misamaha ya kodi kuzidi asilimia moja ya Pato la Taifa na kurekebisha Sheria ya Ukaguzi ya umma wa mwaka 2008 ili kumpa mamlaka ya kisheria CAG kukagua misamaha ya kodi na kuweka wazi matokeo ya ukaguzi huo kwa umma.

Kodi kwa Wafanyakazi

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha ametangaza nafuu ya kodi kwa wafanyakazi wa kima cha chini kutoka kiwango cha 13% mpaka 12%. Kiwango hiki ni kidogo mno na hakimsaidia mfanyakazi kubakia na fedha kwa ajili ya matumizi yake na pia kwa ajili ya kujiwekea akiba. Ni dhahiri kuwa PAYE ni chanzo kikubwa sana cha mapato ya ndani ya Serikali. Kwa mfano mwaka 2013/14 Serikali ilitarajiwa kukusanya tshs 1.5 trilioni kama PAYE ambapo tshs 1 trilioni kutoka idara ya walipa kodi wakubwa na tshs 500 bilioni kutoka idara ya kodi za ndani. Hata hivyo, utaona kuwa mapato haya ni sawa sawa na kodi inayosamehewa kupitia misamaha ya kodi hivyo iwapo misamaha ya kodi ikipunguzwa mpaka kiasi cha asilimia 1 ya Pato la Taifa, Serikali itakusanya kodi ya kutosha kuzipa pengo la punguzo la kodi kwa wafanya kazi. Vile vile Serikali inapoteza kodi nyingi sana kupitia ukwepaji kodi unaofanywa na makampuni makubwa ya kimataifa yanayowekeza hapa nchini (tax evasion and tax avoidance) kwa kiwango cha asilimia 5 ya Pato la Taifa. Iwapo Serikali itajiunga na mikataba ya kimataifa ya kupambana na ukwepaji kodi na pia kuimarisha kitengo cha kodi za Kimataifa ili kupambana na Multinational Corporations ambao wanatumia njia mbalimbali kuhamisha faida zao nje, kutangaza hasara hapa nchini na kukwepa kodi za thamani ya zaidi ya shilingi trilioni mbili kila mwaka kwa mujibu wa takwimu za Global Financial Integrity. Napendekeza kuwa kiwango cha chini cha kipato (mshahara) kukatwa kodi kiwe shilingi 330,000 na kiwango cha chini cha kodi kiwe asilimia 9 tu.

Mheshimiwa Spika, Kiwango hiki cha kodi pia kinawezekana kwa Serikali kuchukua hatua dhidi ya matumizi mabovu ya Serikali. Kwa mfano, kwa mujibu wa Taarifa ya  Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Serikali mwaka 2013, mfumo wa kukagua utumishi wa umma umegundua kuwa jumla ya wafanya kazi wa Serikali 6500 walikuwa wameajiriwa mara mbili kwa majina yale yale, 2700 mara tatu na kulikuwa na watumishi 2500 waliokuwa wanachukua mishahara miwli mpaka mitatu kila mwezi. Baada ya mfumo wa Lawson kuanzishwa jumla ya wafanyakazi  hewa 14,000 waligundulika katika jumla ya wafanyakazi 478,000 wa Serikali. Hatua ya kuondoa matumizi mabovu kutokana na kulipa mishahara hewa pia inaweza kusaidia kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi nchini. Serikali hutumia wastani wa shilingi bilioni 360 kila mwezi kulipa mishahara ambapo katika hizo shilingi bilioni Kumi kila mwezi zimekuwa zikilipwa kwa watumishi hewa. Nafuu ya kodi kwa wafanyakazi nchini katika sekta zote na hasa wafanyakazi wa kima cha chini kitachochea matumizi binafsi ya bidhaa na huduma na hivyo kuchangamsha uchumi na kuwezesha uwekaji wa akiba nchini. Nashauri ukaguzi zaidi ufanyike katika utumishi wa umma ili kumaliza kabisa tatizo la wafanyakazi hewa nchini.

Mheshimiwa Spika ninapongeza kuanzishwa kwa kodi ya zuio kwa ada kwa Wakurugenzi wa makampuni na Mashirika. Kodi hii itaongeza mapato ya Serikali. Hata hivyo kodi kama hii pia itozwe kwenye posho ambazo viongozi wa kisiasa na watumishi wa Serikali wanalipwa isipokuwa posho ya kujikimu (per diem). Vile vile uamuzi wa kuagiza Wizara, Idara na Wakala za Serikali kukusanya maduhuli kwa kutumia mashine za kielektroniki ni uamuzi muhimu sana ambao utaongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi. Kamati ya PAC iliagiza jambo hili tangu mwaka 2013 na ninaamini kuwa Polisi wa Usalama barabarani wataanza kutoa ‘traffic notifications’ kwa njia hii; pia Wizara ya Ardhi wataanza kutoa Hati za Ardhi za kielektroniki na kukusanya maduhuli kwa njia hii ikiwemo Wizara ya Nishati na Madini kwa tozo mbalimbali wanazotoza. Juhudi zote hizi lazima zionekane kwa kupunguza mzigo wa kodi kwa Wafanyakazi ambao kiukweli ni wachache (takribani 1.3 milioni) lakini wanabebeshwa mzigo mkubwa wa kodi kuliko wawekezaji wakubwa.

Mheshimiwa Spika, Tanzania haiwezi kuendelea kuwa nchi ambayo Serikali yake inaendeshwa na fedha za wafanyakazi, wafanyabiashara wadogo na wahisani. Ni lazima makampuni makubwa ya uwezekaji nchini yashiriki kuendesha Serikali kwa kulipa kodi stahili na kuondoa kabisa misamaha ambayo haina mahusiano yeyote na ukuaji wa ajira nchini na kuongeza thamani ya mazao yetu ya kilimo. Vile vile ni muhimu sana kuongeza juhudi za kukuza ajira ili kuwa na wafanyakazi wengi ambao watapelekea kuongeza mapato ya Serikali badala ya kukamua kundi dogo lililopo hivi sasa. Nchini Kenya kiwango cha chini cha Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi (PAYE) ni asilimia 10 tu kwa sababu idadi ya walipaji wa kodi hii wanafikia takribani milioni kumi wakati Tanzania ina wafanyakazi wanaolipwa mishahara ya kila mwezi milioni 1.3 tu.

Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa inaonesha kuwa Tanzania ina jumla wa mifuko mitano ya Hifadhi ya Jamii yenye wanachama 1.3 milioni pekee. Idadi hii ya wanachama ni 6% ya nguvu kazi ya Tanzania. Hata hivyo nguvu kazi ya nchi haipo kwenye wafanyakazi wa mishahara pekee kwani asilimia takribani 70 ya Watanzania wanaishi vijijini na kujihusisha na sekta ya Kilimo. Kwa kuwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii haijafikia wakulima maana yake Watanzania wengi sana wanaishi ya mashaka kwa sababu hawana Bima ya Afya, hawana mafao mengine ya muda mfupi na wala hawana pensheni. Hali hii ni lazima kuirekebisha kama tunataka Taifa lenye maendeleo. Hifadhi ya Jamii sio suala la pensheni tu bali pia ni suala la uwekezaji wa akiba (savings) na uwekezaji wa ndani (investments).

Mheshimiwa Spika, Kasi ya ukuaji uchumi na uwekezaji (Growth and investment rates) vina mahusiano chanya.Takwimu za Penn World Tables (2002) zinaonyesha kuwa kwa nchi 38 za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara wastani wa ukuaji uchumi ulikuwa  0.6% na wastani wa uwiano wa uwekezaji na ukuaji uchumi ulikuwa  10%. Kwa nchi 9 za Asia (9 Asian ‘miracle’ economies), wastani wa ukuaji uchumi ulikuwa 4.9% na wastani wa uwiano kati ya ukuaji uchumi na uwekezaji ulikuwa 25%. Kasi ya ukuaji wa uchumi wa Taifa lolote duniani unahusiana moja kwa moja na utayari wa wananchi wa nchi hizo kuweka akiba na kuwekeza vitega uchumi. Takwimu hizi zinaonyesha dhahiri kwamba ili Afrika ipige hatua ni muhimu sana kuimarisha uwekezaji wa ndani ambao unatokana na kiwango cha uwekaji akiba.

Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi wa kasi na haraka hauwezekani bila ya sekta ya fedha iliyokita mizizi. Hata hivyo, kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Umasikini nchini (PHDR 2009) mfumo wa kibenki nchini kwetu hautoi msaada wa kutosha kwa wafanyabiashara ndogondogo na wakulima. Mikopo kwa uwekezaji wa ndani ni midogo sana kiasi kwamba haisaidii kuongeza uzalishaji (productivity) na kuhimiza mabadiliko makubwa ya Uchumi (transformation of the economy). Mikopo mingi inayotolewa na mabenki ni kwa matumizi binafsi ya watu na mikopo mikubwa ni kwa shughuli za uchuuzi (trading) badala ya uzalishaji. Hii inathibitishwa na Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2013 ambayo inaonyesha kuwa katika mikopo ya thamani ya tshs 10.3 trilioni, ni asilimia 9 tu iliyokwenda sekta ya kilimo. 11.4% viwanda na 25% ilikwenda kwa wachuuzi. Asilimia 17 ya mikopo ilikwenda kwa watu binafsi kwa ajili ya matumizi binafsi!

Kuna haja kubwa ya kufanya mabadiliko makubwa sana ya kimuundo na kisheria na kisera ili kuhakikisha kuwa uzalishaji kwenye kilimo na uongezaji thamani wa bidhaa za kilimo unapata uhakika wa fedha za mikopo. Benki sio rafiki ya Masikini. Benki sio rafiki ya mkulima mdogo hapa nchini. Lazima kubadilika kifikra na kuachana na mazoea. Ni lazima sasa kuweka vivutio kwa wakulima kuweka akiba ya muda mrefu na kuondoa mwiko wa mkulima kutokuwa na pensheni. Hifadhi ya Jamii kwa Mkulima ni suluhisho la kuongeza akiba nchini, kupanua fursa za uwekezaji wa ndani tena kwenye kuongeza uzalishaji wa Kilimo na kujenga jamii ambayo inahifadhiwa. Hifadhi ya Jamii kwa Mkulima pia itaongeza ushindani dhidi ya mabenki katika soko la mikopo midogo midogo na hivyo kumfaidisha mkulima.

Mheshimiwa Spika, mabilioni ya fedha tunayoona yanamilikiwa na mabenki, mifuko ya hifadhi ya jamii, kampuni za bima na asasi za uwekezaji ni matokeo ya kukusanya viakiba vya mtu mmoja mmoja kutoka kwa mamilioni ya watu. Kazi ya asasi za fedha ni kukusanya mabilioni haya na kuyaelekeza kwenye uwekezaji wa miradi mikubwa ianyofanywa na wafanyabiashara na hata miradi midogo kwa wafanyabiashara wadogo. Katika bara la Afrika, hivi sasa watu masikini wanaweka akiba zao katika vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS). Hii ni hali halisi Tanzania, hali ambayo lazima tuijenge kwani mabenki hayapendi kuendesha akiba ndogondogo za watu masikini. Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeanza mafao ya mikopo kwa SACCOS za wanachama wao na hivyo kuweza kukopa kwa lengo la kuendesha maisha yao kwa kuongeza uzalishaji hasa kwenye Kilimo. Wafanyakazi wa Sekta rasmi wametungiwa sheria kwamba ni lazima sehemu ya mishahara yao wakatwe kama akiba ya uzeeni na majanga mengine. Waajiri wao pia hukatwa fedha kuchangia pensheni za wafanyakazi wao. Mkulima hana sheria ya kumlazimisha kuweka akiba (na sio lazima kuwepo kwa sheria hiyo) na pia hana ‘mjomba’ wa kumchangia sehemu ya pensheni yake. Hata hivyo Mkulima anachangia 25% ya Uchumi wa Tanzania (GDP) na pia fedha za kigeni. Mchango wa bidhaa za kilimo kwenye mauzo nje umekuwa mdogo kwa sababu wakulima wananyonywa na mabenki na hawana fursa ya mikopo ya kupanua mashamba yao, kununua pembejeo na kufikia masoko mazuri ya bidhaa zao.

Mheshimiwa Spika, Hali ya Uchumi wa Taifa 2013 inaonesha kuwa 20% ya mapato ya fedha za kigeni nchini yanatoka kwenye bidhaa za kilimo ambacho ni Pamba, Kahawa, Tumbaku, Chai, Korosho, Karafuu na Katani. Mazao haya yanaingiza jumla ya dola za kimarekani 867 milioni. Uchumi wetu hauwezi kuondoa umasikini kwa sababu shughuli zake zimejikita kwenye sekta ya madini ambayo inachangia ajira kiduchu (an enclave) lakini inachangia 40% ya mauzo nje. Uchumi wetu ni egemezi na tegemezi kwa sekta moja tu jambo ambalo ni hatari sana kwa ustawi wa maisha ya wananchi. Ni wajibu wa Serikali kuweka mazingira ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya Kilimo na hivyo kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuondoa umasikini vijijini. Mauzo ya bidhaa za kilimo nje yameshuka kwa kiwango cha asilimia 9, zao la Tumbaku ambalo ndio linaongoza kwa kuingiza fedha za kigeni dola za marekani 307 milioni (zaidi ya shilingi bilioni 500 za kitanzania), mauzo yake yaliporomoka kwa kiwango cha asilimia 12 kutokana na wakulima kutotumia mbolea kwa sababu ya kukosa mikopo katika mabenki kulikosababishwa na unyonyaji wa zaidi ya shilingi bilioni 28 kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi. Mauzo ya Pamba yalishuka kwa asilimia 32 kutokana na mgogoro wa bei uliosababishwa na kutokuwepo kwa sera ya kufidia bei kwa wakulima (price stabilisation).

Mheshimiwa Spika, suluhisho la mambo yote haya ni kuingiza wakulima kwenye hifadhi ya jamii ili waweke akiba, wapate mafao ya muda mfupi na mrefu na wapate mikopo kupitia vyama vyao vya ushirika vya kuweka na kukopa(AMCOS). Mabenki hayataendelea tena kunyonya wakulima kwa sababu riba zinazotolewa kwa mikopo ya SACCOS/AMCOS ni nafuu na zinaendana na hali halisi ya wakulima. Kupitia kujiunga kwao katika Hifadhi ya Jamii, Fao la fidia ya bei laweza kuanzishwa ili kuwafidia wakulima pale bei za mazao yao zinaposhuka chini ya gharama zao za uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, katika jimbo langu la uchaguzi tumefanya mradi huu na hivi sasa wakulima wa kahawa wa vijiji vya Matyazo, Mkabogo na Rusaba kupitia chama chao cha Ushirika cha RUMAKO ni wanachama wa NSSF na tayari wameanza kufaidika na mafao kama bima ya afya na mikopo yenye riba nafuu. Kufuatia mafanikio ya RUMAKO vyama vingine vya ushirika vinavyounda chama kikuu cha KANYOVU chenye vyama 12 vya msingi wamejiunga na NSSF. Tunaweza kusema kwa uhakika kabisa kuwa wakulima wote wa kahawa wa mkoa wa Kigoma wanahifadhi ya Jamii kupitia vyama vyao vya ushirika. Shirika la NSSF sasa limeanzisha mpango wa kuandikisha wakulima wengi zaidi nchi nzima kupitia ‘Wakulima scheme’. Katika mpango huu NSSF wameshirikiana na Tume ya Ushirika nchini ambayo kuanzia january, 2014 imepewa jukumu la kudhibiti na kusimamia vyama vya ushirika nchini. Ni hatua ya kupigiwa mfano. Hata hivyo bila vivutio vya serikali wakulima hawatajiunga na hifadhi ya jamii kwa wingi tunaoutaka ili kubadilisha kabisa uchumi wa watu wetu vijijini.

Mheshimiwa Spika, Napendekeza ifuatavyo;

Serikali ianzishe mpango wa kuwachangia wakulima wanaojiunga na Hifadhi ya Jamii kwa uwiano wa theluthi ya michango yao. Kwa mfano iwapo mkulima atachangia tshs 20,000 kwa mwezi basi Serikali imchangie tshs 10,000 kwa mwezi kwa sharti kwamba iwapo atajitoa kwenye hifadhi ya jamii huu mchango wa Serikali hataupata lakini iwapo akikaa kwenye hifadhi ya jamii kwa miaka isiyopungua kumi/umri wa kustaafu ataweza kupata michango yote na mafao stahiki kwa mujibu wa sheria kama mfanyakazi wa sekta rasmi.
Serikali iachane na mpango wa kuanzisha ‘price stabilisation fund’ na badala yake iweke sera kwamba wakulima waliokwenye Hifadhi ya Jamii moja ya fao watakaolipata ni fao la fidia ya bei ambalo litalipwa kwa namna ambayo wataalamu wa ‘actuarial’ wataona ni endelevu.
Serikali kupitia Msimamizi wa Hifadhi ya Jamii nchini (SSRA) waelekeze kuwa mifuko itenge angalau 40% ya akiba wa wakulima kwenye uwekezaji wa kuendeleza miundombinu ya kilimo, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima kupitia SACCOS/AMCOS
Mheshimiwa Spika, iwapo kwa mfano wakulima milioni moja tu nchini walio kwenye vyama vya Ushirika wakijiunga katika hifadhi ya jamii na kuchangia kiwango cha chini kabisa cha tshs 20,000 kwa mwezi (michango itakayokatwa kulingana na msimu wa kilimo cha zao husika) na serikali kuweka kivutio cha tshs 10,000 katika kila mchango wa mkulima mmoja mmoja katika idadi hiyo, jumla ya Michango itakayokusanywa nitakuwa ni tshs 360 bilioni. Wakulima hawa watapata bima ya afya wao, wenza wao na wategemezi 4 na hivyo bima ya afya kufikia Watanzania milioni 6. Fedha hizi zitatumika kuwekeza kwenye miradi ya uzalishaji katika sekta ya kilimo ikiwemo mikopo ya pembejeo, ujenzi wa miundombinu ya kilimo na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo. Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaweza kuwekeza fedha hizi kama hisa kwenye Benki ya Kilimo na kuwezesha uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo. Hii ndio inaitwa ‘Transformation’.

Mheshimiwa Spika naomba kuwasilisha

Kabwe Zuberi Zitto, Mb

Kigoma Kaskazini.

Kigoma. Juni 17, 2014.