MCHAKATO wa uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) unaanza rasmi Septemba 30 mwaka huu kwa uchukuaji fomu kwa wagombea.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, fomu kwa waombaji uongozi zitaanza kutolewa Septemba 30 mwaka huu, na mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu hizo ni Oktoba 4 mwaka huu.
Fomu hizo zinapatikana ofisi za TAFCA zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 alasiri. Ada ya fomu kwa waombaji wa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Katibu Msaidizi ni sh. 200,000.
Nafasi zilizobaki za Mhazini, mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wajumbe wa Kamati ya Utendaji, ada ya fomu ni sh. 100,000. Uchaguzi wa TAFCA umepangwa kufanyika Novemba 10 mwaka huu.
Na vilevile Klabu za Ligi Kuu na mdhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom zimekutana jana (Septemba 27 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo yalilenga kipengele ya upekee (exclusivity) kilichopo kwenye mkataba wa udhamini ambacho kitaendelea kuwepo. Klabu zilikuwa zimeomba kwa mdhamini kuangalia uwezekano wa kukiondoa.
Pande hizo zimekubaliana kuunda kamati ya pamoja kwa ajili ya kuitafutia kila klabu mdhamini binafsi kwa lengo la kuhakikisha zinashiriki kikamilifu katika ligi hiyo.
Klabu zote zimeshapata vifaa kutoka kwa Vodacom ukiondoa African Lyon ambayo ilitarajia kuchukua vifaa hivyo leo kutoka kwa mdhamini wa ligi hiyo.