Mbunge Zitto Kabwe Matatani..!

Mbunge Zitto Kabwe


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ameingia matatani, baada ya kutakiwa kukanusha tuhuma alizozitoa bungeni katika Mkutano wa Tisa wa Bunge, kwamba mfanyabiashara wa kigeni, Moto Mabanga, alipewa vitalu vya mafuta kinyume na taratibu.

Mfanyabiashara huyo amesema kuwa iwapo Zitto atashindwa kukanusha tuhuma hizo, atafikishwa mahakamani.
Barua iliyoandikwa kwenda kwa mbunge huyo iliyosainiwa na Mwanasheria wa Mabanga, Lawley Shein wa Kampuni ya Uwakili ya Lawley Shein Attorneys, ambayo Mwananchi Jumapili limeiona, inaeleza kuwa hoja binafsi aliyoitoa Zitto, haikuwa na ukweli wowote.

Barua hiyo ya tarehe 28 Novemba, 2012 ilisema kuwa hoja hiyo ya Zitto ni ya uongo, imemkashifu mteja wao na kumshushia hadhi yake binafsi na biashara zake.

“Katika kuthibitisha kuwa tuhuma zako siyo za kweli katika hoja uliyotoa, umemtaja mteja wetu kama raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mteja wetu ni raia wa Afrika Kusini, lakini, umeamua kumtaja kama raia wa Kongo bila kuangalia ukweli,” alisema Shein.

Katika barua hiyo, Shein pia amesema kuwa Zitto amemtuhumu mteja wake Mabanga kuwa aliwahonga baadhi ya vigogo serikalini na kuwapa rushwa wanasiasa katika mchakato wa kufanikisha upatikanaji wa vitalu hivyo.
“Tuhuma hizo siyo za kweli, mteja wetu alifuata taratibu zote kwa uwazi na mamlaka husika nchini na hakuwahi kutoa rushwa kwa mtu yeyote,” alisema mwanasheria huyo.

“Tuhuma hizi ni za uongo, zimemharibia jina mteja wetu na kumsababishia madhara. Kama hutazifuta kauli hizo, uongo huo utamsababishia mteja wetu madhara makubwa zaidi na tutalazimika kudai fidia,” Shein alionya kupitia barua hiyo.

Shein aliongeza kuwa pamoja na Zitto kuongea hoja hiyo akiwa bungeni hivyo kuwa na kinga ya kibunge, lakini kwa mazingira aliyotolea hoja hiyo alitumia vibaya kinga ya kibunge, anayopata mbunge yeyote anapotoa hoja akiwa bungeni.

Kupitia barua hiyo, Shein alimtaka Zitto kufuta kauli yake dhidi ya mteja wao na kwamba mteja wao ana haki zote za kushtaki dhidi ya h

Kupitia barua hiyo, Shein alimtaka Zitto kufuta kauli yake dhidi ya mteja wao na kwamba mteja wao ana haki zote za kushtaki dhidi ya hoja hiyo.

Zitto azungumza.
Alipotakiwa kuzungumzia hoja hiyo na hatua atakazochukua, Zitto alisema kuwa amemwandikia barua Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, kumjulisha hatua hiyo ya kutaka kushtakiwa.

“Nimemwandikia Katibu wa Bunge kumjulisha kwamba nimeletewa kusudio la kushtakiwa, maana hili ni suala la Kinga ya Bunge,” alisema Zitto na kuongeza:

“Mbunge ana kinga kwa masuala aliyozungumza ndani ya Bunge kwa mujibu wa Ibara ya 100 ya Katiba. Kwa hiyo Katibu (Dk Kashililah), atawajibu hao wanasheria.”

CHANZO: Gazeti Mwananchi Jumapili