MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, CCM mkoani Iringa, Godfrey Mgimwa amepiga marufuku wanafunzi waliofanya mtihani wa taifa wa darasa la saba 2014 kwenda mijini kufanya kazi za ndani (uyaya) kwa madai kuwa kazi hiyo ni aibu kubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Iringa.
Akizungumza katika mafahali ya darasa la saba Shule ya Msingi Kalenga na Kiponzelo jana mbunge Mgimwa alisema Mkoa wa Iringa umekuwa ukisifika kwa kutoa wafanyakazi wa ndani jambo ambalo ni aibu na asingependa jimbo lake la Kalenga kuwa katika orodha ya majimbo yanayosifika kutoa watoto wa kazi za ndani.
Mbunge huyo alisema kuwa kwa muda ambao atakuwepo madarakani atafurahi zaidi kuona wazazi wanawasomesha watoto wao elimu ya sekondari ama elimu ya ufundi ili kuja kuwasaidia mbeleni badala ya kuwaruhusu watoto hao kwenda mijini kutumikishwa kazi na ndani na katika madangulo ambayo yanaweza kuwasababishia kurudi kijijini na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
“Wazazi wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba katika shule zote za msingi jimbo langu la Kalenga ninaomba sana kuungana katika kulijenga jimbo la Kalenga kwa kutowaruhusu watu wenye nia mbaya kuja kukusanya watoto wetu na kuwapeleka mijini katika kazi za ndani na madangulo,”
Kwani alisema kuwa kitendo cha baadhi ya wazazi kutopenda kuwasomesha watoto elimu ya sekondari na kuwaruhusu kwenda kufanya kazi ya ndani si heshima kwa wakazi wa jimbo hilo bali ni aibu kubwa ambayo kama isipo kemewa yaweza kuendelea kujenga dhana ya kuwa mkoa wa Iringa ni kisima cha wafanyakazi wa ndani. Mbunge Mgimwa ambae ni katibu wa wabunge wa mkoa wa Iringa alisema kuwa umefika wakati wa wakazi wa Iringa kuungana pamoja na kuugeuza mkoa huo kuwa ni mkoa wa maendeleo badala ya kuwa mkoa wa kuzalisha wafanyakazi wa ndani.
“Tukiungana pamoja tunaweza kuufanya mkoa wa Iringa kuwa wa elimu zaidi hasa ukizingatia mkoa wetu unaongoza kwa kuwa na vyuo vikuu vingi zaidi kuliko mikoa mingine hivyo fursa tuliyonayo ni vema kuiendeleza kuanzia ngazi ya chini kwa kuhakisha wanafunzi wanaomaliza shule za msingi wanaendelea na masomo badala ya kuwaruhusu kwenda kufanya kazi za ndani mijini,”
Alisema kuwa ni vema viongozi wa vijiji vyote vya jimbo la Kalenga kuweka mkakati wa kuwalinda watoto hao waliomaliza darasa la saba kwa kuhakikisha wanakwenda sekondari na wale ambao hawajabahatika kuchaguliwa basi wanapelekwa katika vyuo vya ufundi kwa faida ya jamii ya wana kalenga badala ya kuwaacha kwenda vijiweni na kufanya kazi za ndani mijini.
Pia mbali ya kuwataka wazazi kuwalinda watoto hao kutochukuliwa na watu kwenda mijini kufanya kazi za ndani bado alitaka wale wote wenye tabia ya kwenda vijijini kukusanya watoto kwa ajili ya kuwapeleka mijini kufanya kazi za ndani na zile za madangulo kuachana na tabia hiyo na kuwa iwapo watabainika basi viongozi wa vijiji, kata na wilaya wasisite kuwachukulia hatua kali kama njia ya kuwalinda watoto hao.
“Tunataka mkoa wa Iringa hasa jimbo langu la kalenga kuwa mfano wa kulinda haki za watoto na kuhakikisha dhana ya Iringa na Kalenga kuwa ni chuo cha uyaya inafutika na kuwa ni chuo cha kuzalisha wasomi ambao watapata kutumika katika wizara mbalimbali nchini…leo ukiangalia wizara mbali mbali hapa nchini wakazi wa mkoa wa Iringa waliopo ni wachache sana ukilinganisha na wakazi wa mikoa mingine hivyo lazima mkoa wa Iringa uje kuwa na idadi kubwa ya watumishi wa wizara mbali mbali nchini”
Katika mafahali hayo mbunge Mgimwa alijitolea kusaidia ujenzi wa choo cha wanafunzi katika chule ya msingi Kalenga kwa kutoa fedha za kununua bati zote 43 pamoja na kusaidia ujenzi wa vyoo vy matundu 18 ya wanafunzi katika shule ya msingi Kiponzelo.
CHANZO; Matukiodaima.co.tz