Mbunge wa Chadema, wanachama wakamatwa

Mbunge wa CHADEMA Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema.

Na Janeth Mushi, Arusha

MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) na wanachama wenzake 19 juzi walikamatwa na Jeshi la olisi mkoani hapa na kushikiliwa kwa muda kwa tuhuma za kufanya maandano na mkusanyiko usio na kibali.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoani hapa, Akili Mpwapwa, alithibitisha
kukamatwa kwa Lema juzi jioni kwa tuhuma hizo, baada ya mbunge huyo kutoka mahakamani kwenye kesi ya kupinga matokeo inayomkabili.

Akili alisema kuwa Lema pamoja na wenzake walifanya maandamano baada ya kuahirishwa kwa kesi yake ambapo maandamano hayo yalianzia eneo la Mahakama Kuu hadi ofisini kwake katika jengo la Mkuu wa Wilaya ya Arusha.

Alidai kuwa mara baada ya kufika nje ya ofisi yake, Lema alianza
kuwahutubia wanachama hao kitendo ambacho kilifanya mkusanyiko usio halali kwani haukuwa na kibali kutoka Polisi.

Hata hivyo, alisema Lema na wenzake wote walipata dhamana ya polisi na wanatakiwa kuripoti Makao Makuu ya Polisi Mkoa, kesho kwa mahojiano zaidi juu ya tukio hilo.