Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekanusha taarifa zilizozaa kwenye mitandao kuwa Mbunge wa Viti maalumu kupitia chama hicho, Leticia Nyerere, amekamatwa na uhamiaji kwa kosa la kukiuka masharti ya Green Card na kusema kuwa hayo ni majungu ya kukichafua chama.
Akizungumzia tuhuma hizo jana, Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, Dk. Willibrod Slaa, alisema taarifa hizo ni za uwongo na hazina ukweli wowote ndani yake.
Alisema,amewasiliana na wanachama na wapenzi wa Chadema walioko ndani ya nchi na nje na kusema kuwa Leticia hajakamatwa.
Aliongeza kuwa, taarifa hizo zilizozagaa zinalengo la kukichafulia chama ndani na nje ya nchi kwa sababu wanachama wa chama hicho wanatarajia kufanya mkutano wao Washington DC Marekani siku chache zijazo.
“ Wanachama wa Chadema waishio Washington DC Marekani wanatarajia kufanya mkutano huko na wabunge watatu kutoka nchini watakwenda kuhudhuria mkutano huo,” alisema Dk. Slaa.
Naye Leticia Nyerere, alisema kuwa taarifa hizo si za kweli na anazikanusha vikali.
“Napenda kuchukua nafasi hii kukanusha vikali taarifa iliyosambazwa kupitia Jamii Forum kwamba Leticia Nyerere amekamatwa. Kwa kweli hizi taarifa si za kweli. Ni za uzushi na kutaka kuchafuana.
Tunalaani vikali kwa mtu yeyote aliyehusika na kueneza taarifa hizi za kizushi zisizokuwa na msingi wowote,” alisemaLeticia Nyerere.
CHANZO: NIPASHE