Mbunge wa CHADEMA amlipua Sitta

Spika Mstaafu, Mh. Samuel Sitta

Na Debora Sanja, Dodoma

SPIKA wa Bunge mstaafu, Samuel Sita, amelipuliwa bungeni baada ya Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa, kuhoji uhalali wake wa kuishi katika nyumba ya Spika wa Bunge wakati yeye si Spika.

Msigwa alimlipua Sitta bungeni jana, wakati akiuliza swali katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Alisema wakati Sitta akiwa Spika, alipangishiwa nyumba na Serikali eneo la Masaki, ambapo inakadiriwa alikuwa analipiwa Sh milioni 12 kwa mwezi.

“Kwa kuwa wakati Mheshimiwa Samueli Sitta akiwa Spika katika Bunge la tisa alipangishiwa nyumba eneo la Masaki ambapo inakadiriwa kuwa alikuwa analipiwa Shilingi milioni 12 kwa mwezi,” alisema Mchungaji Msigwa na kuongeza:

“Kwa kuwa hivi karibuni alisafiri kwenda India akiwa na mwenzi wake na msaidizi wake kwa daraja la kwanza. Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Sitta alipangishiwa nyumba kutokana na hadhi yake, na sasa si Spika, bali ni Waziri tu wa Afrika Mashariki, lini Serikali itamuamuru Sitta aondoke Masaki ili akajiunge na wenzake kule Kijitonyama.

“Vilevile ningependa kujua lini Serikali itamzuia yeye na msaidizi wake kusafiri daraja la kwanza kwa kuwa yeye si Spika tena ili kuweza kubana matumizi ya serikali.”

Mara baada ya Msigwa kuuliza swali lake, Spika wa Bunge, Anne Makinda, hakuruhusu lijibiwe kwa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu haihusiki kuwahudumia maspika wastaafu.

“Wakati mwingine ndio maana mnasema huwa nawaingilia, Msekwa (Pius Msekwa) na Sitta ni maspika wastaafu na wanahudumiwa na Bunge kwa mujibu wa masharti ya Spika, huduma hizo ni pamoja na gharama zote zikiwemo matibabu, Waziri Mkuu hahusiki,” alisema Makinda.

Wakati huohuo, Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Mwanamrisho Abama, ameiomba Serikali kutoa baraka zake ili Muungano uvunjwe.

“Kabla sijauliza swali langu nomba nimnukuu Hayati Abeid Karume, alisema Muungano wetu ni kama koti, likikubana waweza kulivua, mimi naona ni wakati muafaka wa kulivua koti hili.

“Muungano umekuwa na migogoro na malalamiko kutoka pande zote mbili, je, Serikali haiwezi kutia baraka zake ili muungano huu uvunjwe,” aliuliza Abama.

Akijibu swali hilo, Pinda, alisema pamoja na Muungano umekuwa na matatizo, lakini njia nzuri ni kukaa na kuangalia jinsi ya kuyatatua.

“Muungano wetu umetuletea heshima kubwa kama Taifa. Lakini kwa sasa tupo katika mchakato wa katiba mpya, kama fikra zako hizi ndio fikra za wote basi tuziangalie katika Katiba mpya.

“Rai yangu ni kuendelea kuwa waangalifu kati suala hili la Muungano, Watanzania tupo zaidi ya milioni 44 na Zanzibar wapo milioni moja na kitu, muungano wowote utakaotaka kuziweka nchi hizi mbili katika mazingira yanayofanana itakuwa ni vigumu kuutekeleza,” alijibu Pinda.

Source: Mtanzania