Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho kutokana na kifo cha Mussa Hamisi Silima aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Baraza la Wawakilishi.
Marehemu Mussa Hamisi Silima amefariki leo, Agosti 23, 2011 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea eneo la Nzuguni karibu na Dodoma, iliyohusisha gari alilokuwa akisafiria mbunge huyo Agosti 21, 2011 akiwa na mkewe, Mwanaheri Twalib ambaye yeye alipoteza maisha papo hapo.
“Nashindwa kupata maneno fasaha ya kuelezea ipasavyo huzuni yangu na mshutuko wangu kufuatia habari za kifo cha Mheshimiwa Silima. Hili ni pigo kubwa lisiloweza kuzibika kwa urahisi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, na kwa kweli Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa ujumla,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake na kuongeza,
“Nilimfahamu Marehemu Silima enzi za uhai wake kutokana na utumishi wake uliojaa uadilifu katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kuzitumikia katika Jumuiya ya Wazazi hadi kufikia wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu, Mwakilishi wa Jimbo la Uchaguzi la Uzini na hatimaye Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Baraza la Wawakilishi.”
Rais Kikwete amesema anaungana na familia ya Marehemu Mussa Hamisi Silima katika kuomboleza msiba mkubwa wa Baba na Mama wa familia na anamuomba Mola azipokee na kuzilaza mahali pema peponi roho za Marehemu Mussa Hamisi Silima na Mkewe Mwanaheri Twalib, Amina.
Aidha, Rais Kikwete amesema anamuomba Mwenyezi Mungu awajalie watoto wa marehemu moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya wazazi wao. Vilevile anamuombea kwa Mola dereva aliyekuwa anawaendesha marehemu ambaye amejeruhiwa, aweze kupona haraka na kuungana tena na familia, ndugu na jamaa zake.