Na Anna Nkinda – Maelezo, Ruangwa
MBUNGE wa Jimbo la Ruangwa, Majaliwa Kassim Majaliwa ameanzisha vilabu 102 vya michezo kwa kuvipatia jezi na mipira ili kuhakikisha vijana wa jimbo hilo lililopo mkoani Lindi hawajishughulishi na matukio ya uhalifu. Majaliwa ambaye pia ni Naibu waziri aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa kilele za sherehe za kutimiza miaka 37 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizofanyika katika Kata ya Likunja wilayani humo.
Katika sherehe hizo Mbunge huyo alizipatia timu za mpira wa miguu za Uhuru City na Mbagala City jezi seti moja kwa kila timu na mpira mmoja ambapo timu hizo zilipanda uwanjani na kuchuana yote hiyo ikiwa ni kusherehekea CCM kutimiza miaka 37. Baada ya kumalizika kwa mashindano hayo timu ya Uhuru City iliibuka mshindi wa mabao mawili kwa nunge dhidi ya timu ya Mbagala City.
Naibu waziri Majaliwa pia ameviwezesha vikundi mbalimbali vya ngoma katika wilaya hiyo ambavyo vinajipatia pesa kwa ajili ya kazi ya sanaa na kuweza kujikwamua kiuchumi.
Sherehe hizo zilienda sambamba na maandamano ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi na kupambwa na burudani ya ngoma za asili, kwaya na mziki kutoka kwa wasanii mbalimbali kikiwemo kikundi cha Wanapakaya kutoka wilayani Kilwa na msanii Dogo Doto.