Na Joachim Mushi
MBUNGE wa Tarime kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nyambari Nyangwine amesema walioshambulia msafara wake hivi karibuni wilayani Tarime ni kundi la watu lililoandaliwa na baadhi ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, ambao hawakupenda jimbo hilo kuchukuliwa na CCM.
Nyangwine pia amepinga taarifa zilizotolewa kuwa alishambuliwa na wananchi na kujeruhiwa kisha kulazwa hospitalini, na kudai taarifa hizo zilipikwa na wapinzani wa chama chake ambao ndio wamekuwa chanzo cha migogoro katika jimbo lake.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wanahabari kuelezea sakata zima la msafara wake ulivyoshambuliwa na maasimu wake kisiasa, jambo ambalo amelilaani vikali kwani hatua hiyo ni hatari kiusalama.
Alisema si wananchi wote kwenye mkutano ule ambao walishambulia mkutano wake, bali ni vijana wachache ambao anadai waliandaliwa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA eneo hilo, pia ndio waliotoa taarifa za kupotoshwa.
Alisema anashangaa kuona wapo wambunge wa maneo mengine lakini wamekuwa wakiingilia jimbo lake (Tarime) na kufanya uamuzi mara kadhaa jambo ambalo linazua migogoro isiyokuwa na msingi. “Baadhi ya wabunge kutoka chama fulani (alipobanwa alitaja ni CHADEMA) wamekuwa wakitoka kwenye majimbo yao wanakuja kufanya uamuzi jimboni kwangu…,” alisema Nyangwine.
Akielezea kwa kina juu ya tukio alisema alikuwa safarini jijini Dar es Salaam na kupata taarifa kuwa yalitokea mauaji ya baadhi ya wapigakura wake ambao walitaka kuvamia mgodi kabla ya kupambana na polisi, ambapo katika tukio hilo baadhi ya wananchi walipigwa risasi na kufa.
Alisema baada ya kupata taarifa alirudi jimboni kwake kujua nini tatizo akiwa kama mwakilishi wa wananchi. Baada ya kufika alifanya mazungumzo na Kamati ya Ulinzi ya Wilaya na kupata taarifa kisha kuanza kujadiliana nini cha kufanya juu ya suala hilo.
Aliongeza Kamati ilimjulisha wanataka kuunda tume ili kuchunguza suala hilo kwa kina. Baada ya hapo aliwashauri kabla ya kuunda tume hiyo anaomba akazungumze na wananchi nao watoe maoni yao kuhusiana na suala hilo.
Alisema alianza kutangaza kufanya mkutano ili kuzungumza na wananchi, lakini eneo hilo lilikuwa na mkutano mwingine wa kimila (litongo) hivyo kukubaliana na viongozi hao kuunganisha mikutano hiyo (yaani litongo na wake).
Alidai baada ya kufika kwenye mkutano walianza mabishano baadhi ya watu walihoji kwanini; “kwanini umekuja na watu wa CCM…wazee walikuwa wakiunga mkono baadhi ya vijana wanapinga nisihutubie…,” alisema Nyangwine.
Baada ya hali hiyo walinzi wake ambao walikuwa wane walimtoa eneo hilo na kumuingiza kwenye gari lake, kisha wao wakarudi kwenye gari lao ambalo walikuwa pamoja na waandishi wa habari wa Mara. Alisema hao wakati wanaondoka baadhi ya watu walianza kulikimbiza gari lao na kwa hasira walivamia gari lingine la halmashauri ambalo walilishambulia na kulivunja vioo.