MBUNGE wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM), kwa mara nyingine ameingia katika kashfa nzito akituhumiwa kutaka kumpiga Mbunge wa Viti Maalumu CUF, Moza Abeid ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa wiki ambapo imeelezwa kuwa Nkamia mbali na kutaka kumpiga mbunge huyo, pia alimtolea matusi mazito ya nguoni (gazeti hili haliwezi kuandika).
Kwa mara ya kwanza mbunge huyo aliingia katika kashfa baada ya kutoa kauli bungeni kuwa hazungumzi na mbwa, bali anazungumza na mwenye mbwa kabla ya kuingia katika mzozo na wahariri na baraza la habari aliposema kuwa Jukwaa la Wahariri na Baraza la Habari ni NGOs za kutafuta fedha.
Uchunguzi wa Mwananchi ambao umethibitishwa na Nkamia mwenyewe umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni kutokana na kuzomewa kwa Nkamia katika kampeni za uchaguzi mdogo Kata ya Dalai Wilaya ya Chemba. Kwa mujibu wa wabunge mashuhuda ambao waliliona tukio hilo, ilielezwa kuwa Nkamia, ambaye pia ni mwandishi wa habari, alianza kumshushia matusi Moza wakiwa ndani ya Bunge hadi walipotoka nje alimfuata na kutaka kumpiga.
“Kweli pale jamaa yetu, alitia aibu, hata hivyo kusema kuwa alikuwa amelewa siyo kweli maana mimi namfahamu Nkamia vizuri ila ilikuwa ni hasira tu,” alisema mmoja wa wabunge walioamua ugomvi huo.
Akizungumzia tukio hilo Moza, alisema kuwa wakati akitoka nje ya ukumbi, alipita karibu na kiti anachokaa Nkamia na ghafla akaitwa, lakini akashangazwa na kitendo cha kuanza kurushiwa matusi.
“Kweli Nkamia na mimi tunatoka wilaya moja, lakini siku ile nilishangaa alinitukana matusi ya nguoni kabisa ……… (anayataja), lakini mimi kule sikusema kitu hadi nilipotoka nje alinifuata na mimi hasira ilinishika nikaanza kumjibu akatupa vitabu ili aje anipige wabunge wenzake wakamkamata,” alisema Moza.
Alisema kuwa chanzo cha matusi hayo ilikuwa ni tuhuma kwamba Nkamia alimtuhumu Moza kuwa aliandaa vijana katika Kata ya Dalai wakati wa kampeni za uchaguzi wa udiwani ili wamtukane.
“Hata hivyo, waliomwambia hivyo kwamba niliandaa vijana au nilimtukana walimdanganya kwani mimi wakati huo nilikuwa bungeni, lakini yeye ndiye aliyeniporomoshea matusi katika kampeni hizo na ushahidi wa sauti ninao,” alisisitiza Moza.
Kwa upande wake Nkamia, ambaye kabla ya kuwa mbunge alikuwa mtumishi wa Serikali katika Shirika la Tanzania Broadcasting Corporation (TBC) alikiri kutokea kwa tukio hilo, lakini alikanusha kuingia bungeni akiwa amelewa kama ilivyoaminika na watu. Nkamia alitoa sababu za ugomvi huo kuwa ni kutokana na taarifa kuwa Moza aliandaa kikosi cha vijana wahuni kulishambulia gari la Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kuwazomea viongozi wake akiwemo yeye.
“Ile ilikuwa ni hali ya kawaida kwa binadamu kupatwa na hasira unapoambiwa kitu kama hicho, lakini sina shida na mbunge Moza na wala sioni kama hilo ni tukio kubwa kiasi cha kuandikwa,” alisema Nkamia.
Mbunge Machali, apigwa alazwa hospitali
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma baada ya kupigwa na watu wasiojulikana wakati akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge juzi.
Tukio la kuvamiwa na kupigwa kwa mbunge huyo, lilitokea saa 2.30 usiku wakati akirejea nyumbani kwake eneo la Area ‘E’ karibu na hoteli maarufu ya Summit. Kwa mujibu wa Machali, watu hao ambao idadi yao haikujulikana, walimsimamisha akiwa mita chache kabla ya kuingia nyumbani kwake akiwa na gari yake ndipo wakaanza kumrushia maneno makali na kumtaka ashuke ndani ya gari.
“Sikuweza kuwafahamu na idadi yao sikuipata mara moja, lakini wameniumiza sehemu mbalimbali za mwili na hasa katika mguu wangu wa kulia sehemu ya paja na sehemu ya pua kama mnavyoona,”alisema Machali.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Chama cha NCCR –Mageuzi James Mbatia, alisema ni tukio baya na ambalo limeonyesha kulikuwa na makusudi maalumu ya kufanya hivyo.
“Ni mapema kueleza tukio hilo kwa sasa, lakini kwa mazingira ilivyotokea inatia mashaka makubwa na kweli tuwashukuru vijana wa CBE ambao waliyatoa maisha yao na kuamua kumsaidia vinginevyo wale walikuwa na nia mbaya,”alisema Mbatia.
Hata hivyo, alisema kuwa hali aliyokuwa nayo jana Machali ilikuwa afadhali ukilinganisha na alivyokuwa juzi wakati anapelekwa hospitalini, ambapo alimkuta akiwa amelowa damu mwili mzima kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu hata kumtambua.
Alipotakiwa kueleza kama tukio hilo linaweza kuwa na uhusiano na masuala ya kisiasa, alisema ni mapema kulizungumzia jambo hilo lakini akataka polisi waachiwe kwanza wafanye kazi yao kwani tangu juzi walitoa ushirikiano mkubwa. Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Nassoro Mzee, aliwaambia waandishi wa habari kuwa walimpokea Machali juzi majira ya saa 5:00 usiku na kuwa hadi jana alikuwa akiendelea vizuri.
Wabunge na viongozi wa Serikali jana walikuwa wakimiminika Hospitali ya Dodoma kumjulia hali, ambapo kwa jana asubuhi alikuwepo Mbunge Albart Ntabalima (Manyovu-CCM), Mbunge wa Kasulu Vijijini Zaituni Buyogela (NCCR- Mageuzi) ambaye tangu juzi usiku walikuwa wameambatana na Mbatia hadi polisi na hospitali. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo hadi jana alisema tayari Polisi ilikuwa inawashikiliwa watu wawili wakihusishwa na tukio hilo.
Kamanda Misime aliwataja watu hao ambao alisema ni vibaka kuwa ni Jeremia Mkude (18) na Charles Chikumbili (22) ambapo walikamatwa na misokoto ya bangi na polisi inaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine wawili.
Miongoni mwa waliokamatwa, mmoja Mkude alikamatwa akiwa na jeraha usoni ambalo lilitokana na kipigo kutoka kwa watu waliokuwa wakimsaidia Machali. Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Mkoa Dodoma linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumvamia na kumshambulia Mbunge Machali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema tukio hilo saa 1:00 jioni katika eneo la Area ‘E’ katika Manispaa ya Dodoma wakati akirejea nyumbani kwake.
“Alikutana na vijana wanne waliokuwa wamesimama katikati ya barabara akapiga honi lakini hawakupisha. Aliamua kuwauliza “Jamani mnasimama katikati ya barabara si nitawagonga?” Nao wakamjibu: “Wewe si unajifanya mtoto wa Mbunge, tutakupiga sasa”. Alisisitiza Kamanda Misime.
Kamanda Misime alisema mheshimiwa alipojaribu kupita vijana hao walipiga gari lake. kitu ambacho kilimfanya ashuke ili atazame kama gari hilo limepata uharibifu wowote, ndipo vijana hao wakaanza kumshambulia kwa ngumi na mateke huku naye akijitahidi kujihami.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema askari walipowafanyia upekuzi watuhumiwa usiku huo wa manane walikutwa na misokoto miwili ya bangi.
CHANZO: mwananchi.co.tz