Mbunge Machali amkinga Mbatia dhidi ya baridi kwa uzi wa buibui!!!

 

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Ndg. James Mbatia

 

Na Muhibu Said

Novemba 5, mwaka huu, Halmashauri Kuu (NEC) ya Taifa ya Chama cha NCCR-Mageuzi, ilifanya kikao jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujadili ajenda moja maalum iliyohusu mpasuko ndani ya chama hicho.

Ajenda ya kikao hicho ilitajwa na Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samuel Ruhuza, kwenye kikao hicho.

Ajenda hiyo ilifuatia hatua ya Kamishna wa NCCR-Mageuzi Mkoa wa Tanga, Mbwana Hassan, kwa kushirikiana na Kamishna mwenzake Mkoa wa Arusha, Mzee Sirikwa, kumuomba Mwenyekiti wao, James Mbatia, kutafakari kuhusu uamuzi wa kujiuzulu wadhifa wake ndani ya chama hicho.

Makamishna hao wa NCCR-Mageuzi, walimpa Mbatia sababu moja ya msingi ya ombi lao hilo kwake. Kwamba, wajumbe wengi wa NEC-NCCR-Mageuzi wamepoteza imani naye.

Inaelezwa kuwa makamishna hao walipowasilisha hoja hiyo kwa Mbatia, aliwauliza walikotoa mawazo hayo, ikiwa ni pamoja na kuwataka wataje majina ya watu waliowatuma kufanya hivyo. Makamishna hao waligoma kutaja majina.

Ni katika kikao hicho cha NEC, wajumbe 28 wa halmashauri hiyo walijitokeza hadharani. Hiyo ni baada ya kuthubutu kusaini waraka uliobeba hoja ya makamishna hao ya kutokuwa na imani na Mbatia.

Hoja hiyo imetoa sababu kuu mbili; ya kwanza ikiwa mwenendo wa Mbatia unaodaiwa kuashiria kuwa anatumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo ni pandikizi (wakala) la CCM ndani ya NCCR-Mageuzi.

Hali hiyo inadaiwa kusababisha Mbatia kuitwa ‘CCM B’ na hivyo kudhoofisha uenezi wa NCCR-Mageuzi.

Sababu ya pili, inatajwa na wajumbe hao wa NEC kuwa inahusu ustaarabu wa kawaida tu. Kwamba, tangu Mbatia awe mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, hajawahi kushinda uchaguzi hata mmoja wa ubunge katika majimbo aliyogombea.

Baya zaidi, majimbo yote aliyogombea, umma ulikuwa na imani na upinzani. Lakini haukuwa na imani na Mbatia. Na ndio sababu inaelezwa kuwa wakashinda wapinzani wengine na si Mbatia.

Majimbo hayo ni pamoja na Vunjo. Huko Mbatia aligombea ubunge mwaka 2000, lakini akaangushwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Tanzania Labour (TLP), Jesse Makundi.

Jimbo lingine ni la Kawe. Huko Mbatia aligombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, lakini akabwagwa vibaya na Mbunge wa sasa wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee.

Hivyo, hoja ya wajumbe hao wa NEC-NCCR-Mageuzi ikawa kuwa huo ni ushahidi kwamba, watu hawamwamini Mbatia kama mpinzani.

Lakini zaidi kwa kushindwa huko, anapoteza uhalali wa kuwa ‘kamanda’ wa chama taifa. Yaani, hawezi kutangaza mapambano dhidi ya CCM wala hawezi kuthubutu kusema atapambana na chama hicho kilichoota mizizi sehemu kubwa ya nchi ilhali kwenye jimbo tu ameshindwa.

Lakini pia wajumbe hao wanadai kuwa Mbatia amepoteza hadhi ya kuweza kunadi hata mgombea yeyote wa NCCR-Mageuzi popote ikitokea uchaguzi. Maana hawezi kuuaminisha umma umwamini mgombea anayemnadi ilhali yeye mwenyewe haaminiki anakogombea mara zote.

Kwenye kikao hicho cha NEC-NCCR-Mageuzi, wajumbe walikwenda mbali zaidi. Mmoja wao kutoka mkoani Ruvuma, Henry Mapunda, alidai kuwa ana ndugu yake ni afisa usalama wa taifa.

Mapunda alidai ndugu yake huyo aliwahi kumweleza kuwa Mbatia ni mtu wao na kuhoji sababu za watu wa usalama kutamka hivyo?

Kwa uchache, hicho ndicho kilichojiri katika kikao hicho cha NEC-NCCR-Mageuzi. Mbatia alihudhuria kikao hicho na yote hayo aliyasikia kwa masikio yake.

Ambacho kilitarajiwa na wengi, ni kusikia Mbatia amejibu au atajibu nini kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwake na wajumbe hao wa NEC-NCCR-Mageuzi.

Hiyo ni baada ya yeye mwenyewe (Mbatia) kuomba katika kikao hicho atendewe haki, ikiwa ni pamoja na kupewa nafasi ya kutosha kujibu tuhuma hizo.

NEC ilimpa siku 21 kufanya hivyo, kuanzia tarehe ya kikao hicho.

Lakusikitisha wakati umma wa Watanzania ukisubiri majibu ya Mbatia, Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, kwa mlango wa nyuma, ameibuka na kubadili somo.

Machali anasema tatizo la NCCR-Mageuzi si Mbatia. Ni Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe.

Anadai kwamba, Kafulila, ambaye ni Mkurugenzi wa Uenezi wa NCCR-Mageuzi Taifa, ndiye kinara wa harakati za kumng’oa Mbatia. Anataka uenyekiti wake ili apate fursa nzuri ya kumtengenezea swahiba wake, Zitto njia ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015 kupitia NCCR-Mageuzi!

Ni dhahiri kuwa kinachotengenezwa sasa na Machali hapa, ni mkakati wa kutaka kubadili mjadala kutoka kwenye hoja ya msingi iliyowasilishwa kwenye kikao cha NEC-NCCR-Mageuzi na wajumbe wa halmashauri hiyo ya kutokuwa na imani na Mbatia kama mpinzani.

Machali anataka mjadala sasa uwe ni vita ya tamaa na uroho wa kutaka uenyekiti wa Mbatia ndani ya NCCR-Mageuzi na kugombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015!

Bahati mbaya mimi kama mtazamaji ni miongoni mwa watu, ambao sikutegemea kama Machali ninayemfahamu angeweza kudiriki kufanya hivyo.

Nasema hivyo kwa sababu. Bahati nzuri, Kafulila mara nyingi amesikika akitamka kwamba, hatarijii kugombea uenyekiti na wala hajawahi kutangaza kugombea nafasi hiyo.

Amesikika akisema kwamba, waliotangaza kuwa watagombea uenyekiti kwa kuwa wamekosa imani na Mbatia kama mpinzani, ni Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali na aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Hashim Rungwe.

Machali anajenga dhana nyingine ya kutaka kumgombanisha Kafulila na Chadema. Kwamba, Kafulila anataka uenyekiti ili kuidhoofisha Chadema.

Anasahau kwamba, yeye (Machali), Kafulila pamoja na Mkosamali, majimbo ya uchaguzi waliyoshinda mkoani Kigoma, ni yale yaliyokuwa yakiwakilishwa na wabunge kupitia CCM tu.

Zaidi ya hivyo, kuna habari kwamba, Kafulila alihakikisha NCCR-Mageuzi haisimamishi mgombea ubunge katika majimbo, ambayo Chadema ina nguvu.

Ndio sababu NCCR-Mageuzi haikuweka mgombea katika jimbo la Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini.

Machali hawezi kuwazuga na kuwapotosha watu wote. Na wala bado hajamsaidia kitu Mbatia. Bali anachokifanya ni kuzidi kumgaragaza Mbatia kwenye matope.

Nasema hivyo, kwa sababu. Katika kikao cha NEC-NCCR-Mageuzi, ushahidi mwiingi ulitolewa na wajumbe wa halmashauri hiyo kuthibitisha hoja yao ya kumkataa Mbatia kuwa mwenyekiti.

Miongoni mwa sababu hizo, ni pamoja na ile inyoahusu kesi ya matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa naye (Mbatia) katika jimbo la Kawe. Wajumbe wanadai kuwa Mbatia ameigeuza kesi hiyo kuwa ya NCCR-Mageuzi.

Si wajumbe hao tu, bali hilo limekuwa likisikika pia likisemwa na Ruhuza. Kwamba, kesi hiyo siyo ya chama. Bali ni suala la mtu binafsi.

Hiyo inatokana na wajumbe wa NEC-NCCR-Mageuzi kukataa kufungua kesi kwenye jimbo, ambalo aliyeshinda ni mpinzani kwa vile lengo la wapinzani linatakiwa liwe ni kuongeza idadi ya wabunge wa upinzani katika Bunge.

Mbatia anadai kuwa amefungua kesi hiyo kwa kuwa alichafuliwa kwenye kampeni.

Rungwe, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, amekuwa akisikika akimshauri Mbatia kuwa kama suala ni kuchafuliwa, basi afungue kesi ya kuchafuliwa jina sio kupinga matokeo ya uchaguzi.

Pamoja na kushauriwa hivyo, Mbatia anadaiwa kutokubaliana na Rungwe. Wajumbe wanadai kwamba, lengo la Mbatia ni kutaka Chadema wapoteze jimbo hilo kwa CCM. Hivyo, suala hilo limeachwa kubaki kuwa la Mbatia mwenyewe.

Swali la msingi wanalojiuliza wajumbe wa NEC-NCCR-Mageuzi, ni kwamba kama chama hakitaki kuwafungulia kesi wapinzani, lakini mwenyekiti wake anafanya hivyo, je, anastahili kuendelea kuongoza chama hicho?

Ushahidi mwingine unaotolewa na wajumbe hao wakidai kuwa ni uthibitisho wao kwamba, Mbatia anatumiwa na CCM, unahusu kumkataza aliyekuwa mgombea urais kupitia NCCR-Mageuzi, Rungwe mwaka jana, kuichafua CCM alipohutubia katika Jimbo la Kawe.

Rungwe aliwahi kulithibitishia gazeti dada la NIPASHE JUMAPILI, NIPASHE kuwa alipata kumshtaki Mbatia kwenye kikao cha NEC kuhusu kumkataza kufanya hivyo.

Ushahidi mwingine unaotolewa na wajumbe hao ni kwamba, mwaka 2007, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, baada ya kutangaza orodha ya mafisadi, Mbatia aliibuka na kusema Watanzania wote ni mafisadi, wanatofautiana viwango tu.

Kauli hiyo inadaiwa kuwa iliashiria kuwa na lengo la kupunguza hasira za umma kwa vigogo wa serikali waliokuwamo kwenye orodha ile.

Ushahidi mwingine unaotolewa na wajumbe hao wanadai kwamba, wakati wa Bunge la Bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/2012, wabunge vijana wa upinzani walionyesha uwezo mkubwa wa kuibana serikali bila aibu.

CCM wakawa wanalalamika kuwa wabunge hao vijana hawajui kanuni na wanaleta fujo. Mbatia wanadai kuwa alitoa tamko kuunga mkono propaganda za CCM kwa kudai wabunge vijana hawajui kilichowapeleka bungeni kwa kuwa hawana uzoefu.

Ushahidi mwingine unatolewa na wajumbe hao kuwa Mbatia anatuhumiwa kushawishi wajumbe wa NEC siku zote kuepuka kutoa kauli kali za kupambana na dola kwa madai kuwa yeye anao uzoefu wa namna dola inavyoweza kubomoa chama.

Wanadai Mbatia anatoa mifano; mmojawapo ukiwa unaomhusu Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kwamba alishughulikia NCCR-Mageuzi kutokana na kauli kali.

Kutokana na hilo, wajumbe wanauliza kama wataogopa kupambana na dola, watakuwaje wapinzani? Mbona Chadema wanapambana na dola na wanafanikiwa?

Ushahidi mwingine uliowekwa bayana na wajumbe hao, ni kwamba Mbatia anatuhumiwa kujisifu mara zote kwenye vikao vya NEC kuwa yeye huongea na watu wakubwa serikalini na wote wanamhakikishia kuwa NCCR-Mageuzi ndio chama mbadala, kina sifa muhimu za kizalendo.

Hapa wajumbe wanahoji. Inawezekanaje mtawala unayetaka kumwondoa madarakani akusifie?

Ushahidi mwingine, ambao umewekwa bayana na wajumbe hao, unaeleza kuwa mwaka 2000 wakati Chama cha Wananchi (CUF) kwa kutumia kaulimbiu yao ya ‘Ngangari’, kilikataa kumtambua Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Amani Abeid Karume kwa kuwa uchaguzi ule ulipingwa hata na Jumuiya ya Kimataifa kwa madai kwamba, haukuwa huru na wa haki.

Baada ya CUF kuweka bayana msimamo wao huo dhidi ya ushindi wa Karume, wajumbe hao wanadai kuwa Mbatia alitoa tamko kuwa kutomtambua Karume ni uhaini. Akachukua uamuzi wa kwenda kuweka pingamizi kwa wagombea sita Zanzibar na kusababisha umma wa visiwani humo kupiga kura za maruhani.

Wajumbe hao wanasema mambo yote hayo ni mjadala uliojiri ndani ya kikao cha NEC-NCCR-Mageuzi, baada ya Mbatia kubanwa sana.

Mwisho, kwa mujibu wa kanuni za chama, Mbatia amepewa siku 21 kujitetea dhidi ya tuhuma hizo, ndipo NEC ifanye maamuzi ama kumsamehe au kumsimamisha uongozi na kuitisha uchaguzi ndani ya miezi sita. Mamlaka ya NEC kumsimamisha yanatokana na Ibara ya 21 ya Katiba ya chama.

Machali alipaswa kumsaidia Mbatia kujibu tuhuma hizo ili kumnusuru. Na si kutafuta visingizio (scapegoat)! Anachokifanya Machali ni sawa na kumsitiri Mbatia dhidi ya baridi kwa kumkinga na uzi wa buibui!

Muhibu Said, ni mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE. Anapatikana kwa simu: 0717055551 au 0733055551 au 0755925656. Barua pepe: muhibu72@yahoo.co.uk

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI