Mbunge, John Mnyika na Ufafanuzi Juu ya Hasara ya Usafiri wa Treni Dar

Usafiri wa treni jijini Dar es Salaam

IFUATAYO ni kauli ya mbunge huyo:-

BAADA
ya baadhi ya vyombo vya habari kuandika Desemba 3, 2012 kauli yangu kuwa usafiri wa treni katika jiji la Dar es salaam kwamba kwa sasa unaingiza hasara ya wastani wa shilingi milioni 10 kwa siku tano, wanahabari mbalimbali kupitia simu na baadhi ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii wametaka nitoe ufafanuzi kuhusu madai hayo.

Ieleweke kwamba nilitoa kauli hiyo wakati nikijibu swali la mwananchi kwenye mkutano wa hadhara tarehe 1 Desemba 2012 katika mtaa wa Saranga Jimboni Ubungo ambaye alihoji kuhusu ufanisi wa usafiri wa treni jijini Dar es salaam na hatua nyingine ambazo Serikali inapaswa kuchukua kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es salaam; hivyo katika hotuba yangu nilizungumza masuala mengi na kueleza mapendekezo niliyotoa kwa nyakati mbalimbali ya kuboresha mfumo mzima wa usafiri.

Nilieleza kwamba naunga mkono usafiri wa treni kuwepo jijini Dar es salaam na kwamba katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ilikuwa ni moja ya masuala niliyoahidi wananchi kwamba nitayafuatilia, na wakati huo wa kampeni wapo walionipinga ikiwemo kwa kuzungumza katika mikutano yao ya kampeni na hata katika radio.

Kazi ya mbunge ni kuwawakilisha wananchi katika kuishauri, kuisimamia serikali na kutunga sheria hivyo kwa msingi huo mara baada ya kuchaguliwa nilihoji bungeni kutaka hatua za haraka za kuanzishwa kwa usafiri huo na hatimaye Wizara ya Uchukuzi (wakati huo ikiwa chini ya Waziri Omar Nundu) mwaka 2011 ikajibu kuwa itatumia sehemu ya fedha kwenye bajeti kuanza matengenezo kwa ajili ya usafiri huo kuanza.

Kwa hiyo nilisisitiza kwenye mkutano wa hadhara usafiri huu kuanza mwaka huu 2012 ni matokeo ya kazi ambayo ilishaanza mwaka 2011, na nikawaeleza wananchi kwamba natambua mchango wa Waziri wa sasa Dk. Harrison Mwakyembe katika kuongeza msukumo; hata hivyo niliwaeleza wananchi kwamba kama mbunge bado siridhiki na maandalizi yaliyofanyika na kwamba iwapo mapendekezo yangezingatiwa kwa wakati usafiri huo ungekuwa na mfumo na utaratibu bora kuliko ilivyo sasa.

Hivyo, nikaeleza kwamba nitaendelea kuwawakilisha wananchi katika kuishauri, kuisimamia serikali na kutunga sheria ili kasoro zilizopo za miundombinu na mfumo wa uendeshaji ziweze kuondolewa na nikatoa mfano kwamba usafiri huo kwa sasa unaingiza hasara ya wastani wa shilingi milioni 10 kwa siku tano hali ambayo inaweza kurekebishwa ili kuhakikisha kwamba usafiri huo unakuwa endelevu badala ya kukwama baadaye kutoka na mzigo wa hasara.

Nitoe ufafanuzi wa nyongeza kwamba natambua kuwa uchambuzi wa gharama (wakati mwingine ikiwa ni hasara) na faida (cost benefit analysis) hutumia vigezo tofauti kisiasa, kiuchumi na kijamii na mtazamo wangu wa muda mrefu ambao unaweza kuthibitishwa kwenye michango yangu bungeni na kauli zangu nje ya bunge, usafiri wa umma (mass transport) unapaswa kuwa huduma zaidi ya biashara hivyo suala la kupata hasara ya kifedha wakati mwingine linaweza lisiwe na uzito likilinganishwa na faida ya kupunguza kero kwa wananchi.

Pia, natambua kwamba uwekezaji unaweza ukaanza kwa hasara wakati huduma au biashara haijafikia kiwango cha kutosha cha watumiaji, wateja au uzalishaji wa kuweza kurudisha gharama na pengine kupata faida (loss before breakeven point).

Hata hivyo, kwa hasara hii ya wastani wa milioni 10 kila baada ya siku tano, hali ni tofauti kwa kuwa chanzo chake sio vigezo hivyo hapo juu vya hasara isiyoepukika (ambayo inaweza kufidiwa kwa serikali kutoa ruzuku kwa sababu za kijamii) wala sio kwa sababu ya kuwa na idadi ndogo ya watumiaji; bali ni kutokana na kutozingatiwa kwa baadhi ya masuala ya msingi katika maandalizi kuanzia kwenye ukarabati wa vichwa cha treni, mabehewa na miundombinu ya reli hali ambayo ni wajibu wa mbunge kuiweka wazi na kutaka serikali irekebishe ili huduma iweze kudumu.

Ikumbukwe kwamba kwamba njia ya treni ya kutoka Ubungo mpaka Stesheni ilikuwa inatumika miaka ya zamani na kampuni ya saruji, kampuni ya makasha ya chuma na kampuni zingine chache ikiwa ni njia binafsi (siding) na toka wakati huo iliacha kutumiwa. Nilieleza tangu mwaka 2010 na 2011 kwamba inapaswa kwanza kuimarishwa ili treni iweze kwenda mwendo kasi zaidi na kuongeza idadi ya safari na hivyo kubeba abiria wengi zaidi na kuondoa hasara kutokana na ongezeko la mapato (economies of scale).

Hatua hii ingeenda sambamba na kuweka reli zenye uzito mkubwa zaidi ambazo zingeweza kubeba vichwa vya treni vyenye nguvu zaidi na mabehewa ya ziada ambayo ni maalum kwa usafiri wa mjini, haya ni masuala ambayo utekelezaji wake ungeanza kwa wakati kama nilivyopendekeza usafiri wa treni ungezinduliwa mapema bila ya kuwa na hasara yoyote. Hali hii inaweza kurekebishwa kwa Wizara ya Uchukuzi kuingilia kati kwa kushirikiana na TRL na TAZARA na kufanya uwekezaji unaostahili.

Badala ya kukwepa mjadala huu kuhusu hasara inayopatikana, ni muhimu mjadala ukaendelea ili wananchi wakafahamu ukweli na hatimaye Serikali ikawajibika kuingiza katika bajeti kuagiza treni maalum za usafiri mjini (Diesel Multiple Unit-DMU au Gas Unit-GU) ziweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na kwamba gharama ndogo; iwapo Serikali haitaufanyia kazi ushauri huu ieleweke kwamba italazimika kutoa ruzuku kwa TRL na TAZARA ili kufidia hasara.

Aidha, changamoto zinazoendelea kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi toka vituo vya treni zinadhihirisha haja ya mapendekezo niliyotoa mwaka 2010 na 2011 ya Serikali kuunganisha mifumo ya usafiri wa umma (mass transit) ya reli, mabasi ya kawaida na mabasi ya haraka ili kuweza kuingiliana na kupunguza gharama za usafiri wa umma.

Ili wazo hilo liweze kuratibiwa vizuri, ni muhimu kuwa na chombo kimoja cha usafiri Dar es salaam mathalani Mamlaka ya Usafiri Dar e salaam (MUDA) badala ya utaratibu wa sasa ambapo mabasi ya haraka yako chini ya DART, mabasi ya kawaida yako chini ya UDA (ambayo mpaka sasa iko katika utata na hali tete) huku treni ziko chini ya TAZARA na TRL/RAHCO na wazo la treni za chini kwa chini nalo likija litaanzishiwa chombo chake; hali ambayo inaongeza gharama za uendeshaji na matatizo ya mifumo kutokuingiliana ipasavyo kuanzia wakati wa uwekezaji na uwekaji wa miundombinu.

Bado, hatua nyingi za ziada zinahitajika zenye kugusa Wizara zaidi ya moja, mathalani Wizara ya Ujenzi na Halmashauri za Manispaa zina wajibu wa barabara za pembezoni za kupunguza msongamano, ndio maana hata baada ya kuanza kwa usafiri wa reli, matatizo ya foleni yanaendelea tofauti na kauli zilizokuwa zikitolewa awali. Hivyo, kwa nafasi yangu ya mwakilishi wa wananchi katika kuishauri na kuisimamia serikali na kutunga sheria nitaendelea kutimiza wajibu huo ndani na nje ya Bunge kwa manufaa ya wananchi wa Jimbo la Ubungo na Taifa kwa ujumla.

Wenu katika maendeleo ya nchi na wananchi,

John Mnyika (Mb)
05/12/2012