Mbunge atoa ushuhuda wa Loliondo kikaoni

Mbunge Beatrice Shelukindo

Na Mwandishi Wetu
Kilindi

MBUNGE wa Jimbo la Kilindi, Beatrice Shelukindo, amesema kuponya kwa tiba ya kikombe cha dawa inayotolewa na Mchungaji mstaafu, Ambilikile Mwasapila ‘Babu’ wa kijiji cha Samunge, kunatokana na imani ya mgonjwa.

Mbunge Shelukindo aliyasema hayo juzi mjini hapa alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya shughuli za mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi 2011/12 katika kikao cha Baraza la Madiwani waliokuwa wakipitisha bajeti mpya ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi.

“Mimi nilikuwa na matatizo yangu fulani nikaenda huko kupata kikombe, baada ya kunywa dawa ile nilipona na hadi sasa nipo fiti. Kwa hiyo ile ni imani ya mtu husika kama watu tukikubaliana kwenda, watu waende ila imani iwe mbele,” alisema Shelukindo.

Shelukindo aliyasema baada ya baadhi ya madiwani kuuliza kama kuna uthibitisho kuwa dawa inayotolewa na mchungaji huyo inaponya Ukimwi, ili fedha zilizotengwa na Halmashauri ya Wilaya hiyo kwenye bajeti yake kiasi cha sh. milioni 50.3 zitumike kuwasafirisha wagonjwa wenye Ukimwi kwenda kwa babu badala ya kutumika kwa elimu na mambo mengine kwa wagonjwa hao.

Baada ya majadiliano huo ndipo Mbunge huyo akatoa ushuhuda wake kwa madiwani, akisema yeye alisha kwenda kitambo kupata kikombe cha Babu, na imani yake aliyokuwa nayo dhidi ya ugonjwa uliokuwa ukimsumbua, amepona na sasa hali yake inaendelea vizuri. Hata hivyo Mbunge huyo hakutaja ugonjwa uliokuwa ukimsumbuwa kwenye kikao hicho.

“Tunasikia kwenye vyombo vya habari jinsi watu mbalimbali wanavyomiminika huko Loliondo kupata dawa za magonjwa sugu na tunasikia ati wanapona wakiwemo viongozi wa kitaifa, sasa kama ni kweli basi bajeti hii tuitumie kuwasafirisha wagonjwa wenye Ukimwi ili wakapate kikombe,” alisema mmoja wa madiwani hao na kuungwa mkono na wenzake huku ukumbi ukiripuka kwa kicheko.

Hata hivyo alipotakiwa kulitolea ufafanuzi suala hilo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Dk. Michael Chabai, alisema kuwa, mpaka sasa hajapata uthibitisho kama dawa hiyo inayotolewa Loliondo inatibu ugonjwa huo. Kwamba anachofahamu yeye ni kuwa haina madhara kwa watumiaji tu.

“Waheshimiwa wenzangu hilo la kwamba dawa anayotoa babu inatibu ugonjwa wa Ukimwi, hilo sinataarifa nalo. Hata hivyo bado uchunguzi unafanyika ili kuthibitisha kama waliopata dawa wamepona au laa. Kwa hiyo nashauri tuendelee kuhamasisha wananchi hasa wale wanaotumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo, waendelee na matumizi kwa kuzingatia maelekezo,” alisema Dk. Chabai.