Mbunge Apinga Kuingilia Mkataba wa Tenda Tanesco

Sarah Msafiri wa Viti Maalumu CCM

NA Hii ni taarifa ya mbunge huyo, Sarah Msafiri wa Viti Maalumu CCM akipinga.
ITAKUMBUKWA katika kikao cha Bunge la Bajeti 2012/2013 ziliibuka tuhuma mbalimbali zikiwemo za baadhi ya wabunge wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini kufanya Biashara ya Matairi Tanesco, tuhuma za Wabunge kuomba Rushwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, na tuhuma za kuwepo kwa Makampuni ya Mafuta Kuhonga Wabunge wasipitishe Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini Bungeni.Pamoja na Kamati iliyoundwa na Mhe. Spika kuchunguza tuhuma hizo kufanya kazi yake ambapo watu mbalimbali wakiwemo Wabunge, Watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Tanesco kufika na kutoa maelezo mbele ya Kamati hiyo.

Nimeshtushwa sana na taarifa ya baadhi ya vyombo vya habari kunihusisha mimi na Kampuni ya M/S Sharrifs Services & General Supply iliyokuwa ikifanya biashara na Tanesco na kudai kwamba nilisimamia malipo yenye utata kutoka Shirika la Tanesco.

Ndugu Waandishi,
Kwanza, nimeshangazwa na habari hii ambayo haina hata chembe ya ukweli wowote kwani binafsi sifanyi biashara yeyote na Tanesco, Sina Mahusiano yeyote ya kibiashara na Kampuni ya Sharrifs, Katika kampuni hiyo mimi siyo Mmiliki, mimi siyo Mkurugenzi, Sina Hisa wala Sijaajiriwa kwa kazi yeyote na Sharrifs. Nawataka Wahariri na Waandishi au Mtu yeyote mwenye ushahidi wa malipo hayo ya matairi ajitokeze hadharani na kuwaeleza Watanzania kwani Tanesco ni Shirika la Serikali na kuna taratibu za malipo Serikalini.

Pili, nahoji weledi na uhalali wa baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari bila kuzingatia masharti ya kazi za habari kwa kuandika habari za upande mmoja wanazoziita za watoa taarifa wao bila kunitafuta na kujua maoni yangu juu ya tuhuma hizo.

Tatu, endapo Waandishi wanazo taarifa zisizo na mashaka kwamba nilishiriki wakati wa kufunga Mkataba kati ya Tanesco na Kampuni ya Sharrifs kwanini wameshindwa kutoa nakala ya muhtasari wa kikao hicho cha pande mbili au kielelezo chochote kinachoonyesha ushiriki wangu ili Watanzania wajue ukweli wa habari zinazoandikwa.

Nne, naamini hakuna Mtanzania asiyejua kwamba Mhe. Spika aliunda Kamati Maalum ya Kuchunguza tuhuma mbalambali ikiwemo hii, kwanini vyombo vya habari au Waandishi hawajapeleka Ushahidi huo kwenye kamati iliyoundwa kuchunguza tuhuma hizo? Endapo walishapeleka ushahidi huo basi nawashauri wasubiri ripoti ya Kamati badala ya kuendekeza Majungu.

Ndugu Waandishi,
Ninachojua kuhusu Kampuni ya Sharrifs ni kupitia kwa Mkurugenzi wake Bw. Heri ambaye mimi kama Mbunge alikuja kwangu kunieleza matatizo yake kwamba aliomba Tenda Tanesco kupitia Kampuni yake ya Sharrifs wakashinda Tenda, wakapewa barua na Tanesco ya kujulishwa kwamba wameshinda (letter of award) kisha wakapewa barua ya kwenda kufanya majadiliano pande mbili yaani Tanesco na Sharrifs (letter of negotiation) ambapo baada ya kukamilisha process hizo walipewa Mkataba ambao kimsingi unabeba makabaliano ya mazungumzo waliokaa pande zote mbili yakiwemo jinsi ya kusupply bidhaa, muda wa kusupply na mfumo wa malipo, Kampuni ya Sharrifs wakasaini na kurudisha Mkataba huo Tanesco na kuendelea kusubiri warudishiwe kwa ajili ya Sharrifs kuanza biashara ya kusuppy Tanesco.

Kama Mbunge ambaye ninawajibu wa kushughulikia kero za Wananchi nilienda kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco na kumweleza madai hayo ya Sharrifs, nakumbuka Mkurugenzi alimwita Mkuu wa Idara ya manunuzi ambaye alikiri kuifahamu Sharrifs na Mkataba wake alishaushughulikia na kuupeleka kwa Mwanasheria ambapo baada ya mazungumzo mwanasheria akaomba kwenda kutazama huo Mkataba kwenye ofisi yake, Baada ya muda Mwanasheria alirejea huku akiwa amebeba huo Mkataba ukiwa umefungwa kwenye Bahasha ya Kaki. Nakumbuka Mwanasheria alimweleza Mkurugenzi kwamba Mkataba alishaushughulikia na amejiridhisha uko vizuri.

Nakumbuka Mkurugenzi akawa anamwambia Mwanasheria kwanini anakaa na documents ambazo anatakiwa azipeleke sehemu zinazohusika ili wateja wasipate usumbufu wanapozifuatilia. Tukiwa wote nikampigia simu Bw. Heri na kumweleza niko Tanesco Mkataba wake uko tayari uko kwa Mwanasheria hivyo aje kuuchukua, Bw. Heri akanijibu yeye yuko mbali ila kama itawezekana nimchukulie ataupitia nyumbani kwani ni jirani yangu maeneo ninapoishi.

Nakumbuka kabisa Mwanasheria akasema naweza nikamchukulia huo Mkataba mradi niende nikasaini kwenye kitabu cha dispatch kwa kumbukumbu kwamba mkataba umeshatoka Tanesco. Nami nikafanya hivyo, ambapo jioni Bw. Heri akapitia nyumbani akauchukua ukiwa umefungwa, wala sijui kilichoandikwa ndani wala masharti na makubaliano ya biashara yao.

Aidha sikuwa na haja ya kujua walichokubaliana kwenye Mkataba kwani kwanza hayanihusu, Mkataba ni kati ya Muuzaji na Mnunuzi ambaye ni Kampuni ya Sharrifs na Tanesco. Hivyo nashangaa kuona baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari zisizo na ukweli wowote tena bila kusikiliza maoni yangu juu ya tuhuma hizo ambazo kimsingi zimelenga kunichafua kisiasa. Naomba Waandishi wa habari warejee weledi wa kazi zao, waheshimu Misingi ya Uandishi wa Habari, pia waache kutumiwa na kikundi cha watu ambao kwa makusudi wanataka kupotosha ukweli wa jambo hili.

Nataka Watanzania wajue kwamba huu ni Mkakati uliowekwa wa kunimaliza mimi kisiasa na kuchafua jina langu, Mkakati ambao wamefanikiwa kwa kiasi Fulani. Naomba nirudie tena kwa kuwataka Waandishi kupitia hao watu wao wanaojiita watoa habari wajitokeze hadharani waseme Kampuni ya Sharrifs imekiuka wapi taratibu za tenda (tenda process) kwani kisheria taratibu za tenda ndio zitakazoonyesha endapo mimi Mbunge nimesababisha kuwepo kwa Mgongano wa Maslahi (undo influence or conflict of interests),

Siyo kwamba kwa vile mimi ni Mbunge au Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini nimeenda Tanesco kujua kwanini Sharrifs imeshinda tenda kihalali lakini Mwanasheria anawazungusha kuwapa mkataba wa kuanza kufanya kazi ndio itafsiriwe kwamba ni Mgongano wa Maslahi kama vinavyodai baadhi vya vyombo vya habari.

Nataka niwajulishe Watanzania kwamba kisheria siyo kosa Mbunge kuwa na Kampuni au Kufanya biashara, Hivyo nisingeona ugumu wowote wa kukubali endapo ninamahusiano ya kibiashara na kampuni ya Sharrifs, Aidha kitendo cha kuwa Mbunge hakikufanyi ushinde Tenda, unaweza ukawa na kampuni ukaomba Tenda, ukashindanishwa na ukashindwa. Kwani lazima kampuni ikidhi masharti ya Tenda. Sasa hao wanaosema nina mahusiano ya kibiashara na Sharrifs, nimesababisha mgongano wa maslahi wajitokeze hadharani na ushahidi wao.

Binafsi naamini sijakiuka taratibu zozote wala sikuingilia kazi za Tanesco kwani mimi siyo sehemu ya chombo chochote cha Maamuzi cha Tanesco. Mimi siyo Mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Siyo Mkurugenzi wala Mtumishi wa Tanesco na hakuna sheria wala kanuni inayonizuia kufanya biashara na Tanesco kwa kigezo cha kuwa Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini. Nilikuwa nasimamia majukumu yangu kama Mbunge kwa Mujibu wa Katiba ya Nchi. Kupitia taarifa hii naomba Waandishi wa habari kufanya kazi kwa Utafiti unaoweza kusaidia Jamii katika kupata ukweli wa suala hili badala ya kuandika kwa nia ya kupotosha.

Kupitia taarifa hii, ninaomba wale wote waliochapisha taarifa hizo bila kuwa na uthibitisho wala kutaka kupata maoni yangu nawataka waniombe radhi kupitia kurasa za mbele za magazeti yao kwenye matoleo yanayofuata, Vinginevyo nimeshaongea na Mwanasheria wangu kwa ajili ya hatua za Kisheria.

Sarah Msafiri
Mbunge Viti Maalum (CCM)
Morogoro