Mbunge amuita mkuu wa mkoa mnyonyaji wa wakulima


Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara.

Dodoma,

MBUNGE Seleman Bungara wa Jimbo la Kilwa Kusini (CUF), amediriki kumuita Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Meck Sadiq kuwa ni mnyonyaji mkubwa wa wakulima wa zao la ufuta jimboni kwake.

Mbunge huyo, amesema Sadiq na kundi lake la watu wachache wamekuwa wakiwalazimisha wauze ufuta wao kwenye Chama cha Ushirika Ilulu, ambacho kinanunua kwa bei ya chini ya sh. 1,000 ambayo haina maslahi kwa wakulima.

Bungara alimuomba, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika kutoa tamko la ili kuwaruhusu wakulima wa zao hilo mkoani Lindi kuuza kwa wanunuzi wengine, ambao hununua kwa sh. 1, 500 na si kulazimishwa kama ilivyosasa.

Bungara alitoa kilio hicho mjini Dodoma jana, wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha, ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika kwa mwaka 2011/2012.

“Wakati wa msimu wa kilimo Serikali haitoi msaada wowote kwa wakulima, lakini inapofika kipindi cha kuuza mazao ndipo inajitokeza mbelembele kwa kuwalazimisha wauze sehemu moja pekee tena kwa bei kandamizi. Kikundi cha watu wachache kikiongozwa na Sadiq ni vinara wa kuwanyonga wakulima wa ufuta wa Lindi. Kwanini anawalazimisha wauze kwenye chama cha ushirika ambacho kinanunua kwa sh. 1, 000, sasa huu si unyonyaji,” alisema.

“Nilimwandikia barua Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mkuu wa Wilaya na Waziri wa Kilimo, Prof. Jumanne Maghembe juu ya dhuluma hii nikiwataka waangalie suala la bei ya ufuta, lakini wote wamekaa kimya, na wameshindwa kumaliza tatizo la bei kwa wakulima wa ufuta. Waziri Mkuu anamuogopa mkuu wa mkoa, leo (jana) namtaka, Waziri atoe tamko hapa la kuwaruhusu wakulima wa Lindi wauze ufuta wao kwa sehemu yoyote na kwa wanunuzi binafsi ambao wananunua kwa sh. 1, 500 kwa kilo.
Leo nitatoa shilingi, najua sitashinda kwasababu CCM mpo wengi na kazi yenu nikusema ndiyoooo, na nikishindwa nitaandamana usiku na mchana mpaka nione wakulima wa ufuta wanakuwa huru ingawa maandamano hamyataki,” alisema Bungara.

Mbunge huyo akiendelea kuzungumza alikikebehi Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kusema kuwa chama legelege huzaa Serikali legelege.

“Naishukuru Serikali ya CCM kwa miaka 50 kuendelea kuwa ombaomba, hata mkikipa miaka mingine 50 hali itakuwa mbaya zaidi, hii inatokana na ulegelege wake,” alisema.